2014-10-29 14:56:21

Dr. Guy Scott kuongoza Zambia katika kipindi cha mpito!


Makamu wa Rais Dr. Guy Scott ameteuliwa kuongoza Zambia katika kipindi hiki cha mpito hadi uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa. Rais Guy Scott anachukua madaraka haya baada ya Rais Michael Sata kufariki dunia Jijini London, tarehe 28 Oktoba 2014, akiwa na umri wa miaka 77.

Dr. Scott mwenye umri wa miaka 70 alizaliwa kunako tarehe 1 Juni 1944 huko Livingstone, Kaskazini mwa Rhodesia baada ya wazazi wake kuhamia Zambia kwa sasa ni raia kamili wa Zambia pasi na mashaka yoyote. Nyota yake ilianza kuonekana pale Rais Michael Sata aliposhinda kwenye uchaguzi mkuu nchini Zambia kunako mwaka 2011 na hapo akateuliwa na kuapishwa kuwa Makamu wa Rais kunako tarehe 29 Septemba 2011. Anasema, hakuyaamini macho yake, akadhani kwamba, wananchi wa Zambia walikuwa wanataka kumkejeri!

Dr. Scott ambaye kwa taaluma ni mchumi aliyebobea katika mahojiano maalum na baadhi ya vyombo vya habari anasema kwamba, ataendelea kuimarisha uchumi wa Zambia kwa kukazia sekta ya madini ambayo inaliingizia taifa pato kubwa kutokana na kodi mbali mbali, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, makampuni ya madini yanalipa kodi kama inavyotakiwa. Hakuna sababu ya kubinafsisha mali binafsi, bali ni kuweka sera nzuri za kugawa raslimali na utajiri wa nchi kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, afya na miundo mbinu, ili kutengeneza na kukuza fursa za ajira.

Serikali ya Zambia inataka kujielekeza zaidi katika sekta ya kilimo na utalii, ili kutoa fursa nyingi za ajira kwa wananchi wa Zambia badala ya kuendelea kung'ang'ania sekta ya madini ambayo kwa sasa inatoa ajira "kiduchu". Wananchi wa Zambia wataendelea kuwezeshwa ili kupata mitaji itakayowasaidia kuendesha shughuli mbali mbali za uzalishaji na utoaji wa huduma. Serikali inaendelea kupambana na Taasisi za fedha nchini Zambia ili kupunguza riba kubwa inayotolewa kwa sasa.

Uchaguzi mkuu anasema Bwana Edgar Lungu ambaye alitarajiwa na wengi kushikilia madaraka katika kipindi hiki cha mpito kwamba, utafanyika katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.







All the contents on this site are copyrighted ©.