Vietnam kuwekeza katika usafiri wa maji na teknolojia ya habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili
mjini Hanoi asubuhi, Jumatatu, Oktoba 27, 2014 kuanza ziara rasmi ya siku mbili ya
Kiserikali nchini Vietnam. Rais Kikwete amewasili mjini Hanoi akitokea nchi jirani
ya Jamhuri ya Watu wa China ambako Jumapili, Oktoba 26, 2014 alimaliza ziara rasmi
ya Kiserikali yeye mafaniko makubwa ya siku sita nchini humo.
Kwenye Uwanja
wa Ndege wa Noi Bai mjini Hanoi, Rais Kikwete amepokelewa na viongozi wa Jamhuri ya
Kisoshalisti ya Vietnam na baada ya mapumziko mafupi, Rais Kikwete amekwenda Kasri
ya Kirais kukutana na Rais Truong Tan Sang kwa mazungumzo ya faragha na baadaye kwa
mazungumzo ya Serikali kati ya Tanzania na Vietnam.
Mara baada ya kuwasili
kwenye Kasri hiyo, Rais alipokelewa na Rais Sang na akakagua gwaride la heshima ambalo
liliundwa na Jeshi la nchi hiyo lililokuwa na vikosi vya anga, maji na nchi kavu.
Baada
ya mazungumzo hayo, Marais hao wawili wameshuhudia utiaji saini wa Makubaliano katika
Usafiri wa Majini (Marine Transport) ambao umetiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe kwa niaba ya Tanzania na Waziri
wa Usafirishaji wa Vietnam, Mheshimiwa Dinh Li Thang kwa niaba ya nchi yake.
Mbali
na kukutana na Rais Sang, Rais Kikwete baadaye amekutana na kufanya mazungumzo na
Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam, Mheshimiwa Nguyen Phu Trong, ambaye
pia ndiye kiongozi mkuu wa nchi hiyo. Viongozi hao wawili wamekutana kwenye Makao
Makuu ya Kamati Kuu ya Chama hicho cha Kikomunisti, yanayoangaliana na Kasri ya Rais.
Rais
Kikwete pia amefanya ziara kwenye Makao Makuu ya Kampuni ya Simu ya Viettel ambayo
inajiandaa kuingia katika soko la vijijini katika Tanzania. Wakati wa mazungumzo kati
ya Rais Kikwete na viongozi wa Kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC), Juliet Kairuki ameukabidhi uongozi wa Kampuni hiyo hati ya kuanzishwa kwa Kituo
hicho.
Baadaye usiku, Rais Kikwete amehudhuria Hafla ya Chakula cha Jioni iliyoandaliwa
kwa heshima yake na mwenyeji wake Rais Sang kwenye Kituo cha Kimataifa cha International
Convention Centre mjini Hanoi. Rais Kikwete ataendelea na ziara yake ya Vietnam leo
kwa kutembelea sehemu mbali mbali na kukutana na Spika wa Bunge la Vietnam, Mheshimiwa
Nguyen Sinh Hung.
Hiyo ni ziara ya kwanza kufanywa na Mheshimiwa Kikwete akiwa
Rais wa Tanzania, lakini hiyo ni mara ya pili kwake kutembelea Vietnam. Alitembelea
Vietnam mwaka 2004, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Wakati
huo huo habari zinasema kwamba, kila Mtanzania nchini atakuwa na uwezo wa kupata simu
ya kisasa na yenye uwezo mkubwa (smart phone) kwa bei ya chini kabisa katika miaka
mitano ijayo kuanzia mwaka 2020 kwa mujibu wa mipango ya kampuni mpya ya simu inayojiandaa
kuingia katika soko la simu la Tanzania. Aidha, Kampuni ya Viettel ya Vietnam imemwambia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatatu,
Oktoba 27, mwaka huu, 2014 kuwa itateremsha kwa kiasi kikubwa bei ya simu za kawaida
na smart phone, ili kuwezesha kila Mtanzania kuwa na simu.
Kampuni hiyo pia
imemwambia Rais Kikwete kuwa itasambaza mawasiliano ya internet kwa kila kijiji nchini
na kuwa kwa taasisi za umma kama vile shule, hospitali, vituo vya polisi zitapatiwa
huduma hiyo bila malipo yoyote. Rais Kikwete ameambiwa habari hiyo njema kwa Watanzania
na Mwenyekiti wa Kampuni ya Simu ya Viettel wakati alipotembelea makao makuu ya Kampuni
hiyo mjini Hanoi kwenye siku yake ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Kiserikali katika
Vietnam.
Mwenyekiti wa Kampuni hiyo ya umma ambayo inamilikiwa na Jeshi la
Vietnam, Bwana Nguyen Manh Hung amemwambia Rais Kikwete kuwa Viettel inakusudia kumwezesha
kila Mtanzania kumiliki smart phone kwa kupunguza bei ya simu hiyo na pia kupunguza
bei ya huduma muhimu kama vile ile ya internet.
Bwana Hung amesema kuwa Kampuni
yake inapanga kupunguza bei ya simu za kawaida hadi kufikia dola za Marekani 15, sawa
na shilingi 25,000 na punguza ile bei ya smart phone hadi kufikia dola za Marekani
40, sawa na shilingi 65,000. Sasa hivi, bei ya simu hizo ni kubwa mara nyingi ya kisai
hicho kinachokusudiwa.
“Tunataka kuifanya bei ya kununua smart phone kuwa mara
10 chini ya bei ya kununua kompyuta. Tunasukudia pia kupunguza bei ya matumizi ya
simu kuwa dola moja tu ya Marekani, sawa na shilingi 1,600, kwa watu wa kawaida kwa
mwezi na kwa wale ambao wanatumia simu kwa huduma nyingi zaidi watalipa dola za Merakani
50, sawa na shilingi 78,000, kwa mwezi,” amesema Bwana Hung.
Mwenyekiti huyo
amesema kuwa Kampuni yake itawekeza kiasi cha dola za Marekani bilioni moja katika
huduma za simu na huduma nyingine katika Tanzania na hivyo kuifanya Tanzania kuwa
nchi ya pili nyuma ya Peru kupata mfumo wa simu wa kisasa zaidi miongoni mwa nchi
ambako Kampuni hiyo ina shughuli zake.
Amesema kuwa ndani ya miaka mitatu tokea
Kampuni hiyo kuanza shughuli zake katika Tanzania, kiasi cha vijiji 4,000 ambavyo
kwa sasa havina mawasiliano vitapatiwa huduma hiyo katika awamu ya kwanza.
“Katika
awamu ya pili, kiasi cha vituo 150 vya polisi, hospitali za umma 150, ofisi za Shirika
la Posta kiasi cha 65 nchini vitapatiwa huduma ya mawasiliamo yakiwemo ya internet
bure katika mwaka wa kwanza wa Kampuni hiyo kuanza shughuli zake. Tutatoa pia huduma
ya internet na mfumo wa teknolojia ya mawasiliano bure kwa shule 450 za umma katika
wilaya 150 ambazo tayari zina umeme, huduma ambazo pia zitatolewa katika mwaka wa
kwanza wa Kampuni hiyo kuanza kazi,”amesema.
Bwana Hung amesema kuwa Kampuni
hiyo iliyoanzishwa mwaka 1989 iliingia katika shughuli za simu mwaka 2000 na kuanza
shughuli za simu za mkononi mwaka 2004.Mwaka 2013, mapato ya kampuni hiyo yalikuwa
ni dola za Marekani bilioni 9.1 na kati ya hizo kampuni hiyo ilikuwa imepata faida
ya karibu dola za Marekani bilioni moja.