2014-10-28 09:41:15

Nitawatumikia waamini wa Jimbo Katoliki Kigoma kwa ari na moyo mkuu!


Askofu mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, akisaidiana na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa na Askofu mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, walikuwa wahusika wakuu katika Ibada ya kumweka Wakfu Askofu Josefu Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma, iBada iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji.

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amemhakikishia Askofu Mlola ushirikiano wa dhati kutoka kwa Maaskofu wenzake na kwamba, Jimbo Katoliki la Kigoma lina utajiri mkubwa wa imani iliyopandwa na Wamissionari wa Afrika.

Hii ni fursa kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu pia ni mwaliko wa kukabiliana na changamoto zilizobainishwa katika maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo Katoliki Kigoma, ili kuweza kulipyaisha Kanisa katika maisha na utume wake, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati.

Naye Askofu mkuu Francisco Padilla amemtaka Askofu Josefu Mlola kuonesha ujasiri na umakini mkubwa katika kuubeba Msalaba wa kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza waamini wa Jimbo Katoliki Kigoma. Amemtaka asimamie ukweli, haki na maadili, daima akijitahidi kuwa huru katika utekelezaji wa majukumu yake kama Kiongozi mkuu wa Jimbo Katoliki la Kigoma.

Kwa upande wake, Askofu Josefu Mlola ameahidi kuwatumikia Watu wa Mungu Jimbo Katoliki Kigoma kwa ari na moyo mkuu, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu; ustawi na maendeleo ya Kanisa Jimboni Kigoma.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania katika Ibada hii amewakilishwa na Professa Mark Mwandosya, Waziri wa Ofisi ya Rais asiyekuwa na Wizara maalum, ameelezea umuhimu wa Muswada wa Katiba Mpya ya Tanzania kwamba, unakidhi matakwa ya kidini, ikilinganishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977. Amewataka viongozi wa kidini kusaidia mchakato wa kulinda, kutunza na kudumisha amani nchini Tanzania.

Ibada ya kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa kwa Askofu Josefu Mlola kuwa Askofu wa sita wa Jimbo Katoliki Kigoma, imehudhuriwa na Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Kigoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.