2014-10-27 08:17:07

Yaliyojiri kwenye ziara ya Pinda nchini Poland


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali ya Tanzania inaangalia uwezekano wa kupata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland utakaoliongezea Taifa uwezo wa kuhifadhi chakula tofauti na hali ilivyo sasa Alisema uzalishaji mwaka huu umetoa ziada ya tani milioni 1.5 za nafaka na tani 800,000 za mpunga ikilinganishwa na ziada ya tani 300,000 iliyokuwepo mwaka jana. “Serikali inakabiliwa na changamoto ya kupata soko la uhakika kwa mazao ya wakulima kwa sababu tulizoea kumtumia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kama mnununzi mkuu na uwezo wezo wake ni tani 240,000 tu kwa mwaka,” alisema.
Akizungumza baada ya kutembelea kampuni ya MLYNPOL ambayo inanunua mazao kwa wakulima na kusindika nafaka Ijumaa, Oktoba 24, 2014) Waziri Mkuu alisema teknolojia ya ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhia chakula katika muda mfupi ndiyo suluhisho pekee kwa wakulima wa Tanzania katika kipindi tulichonacho.
“Wenzetu wana teknolojia ya kisasa ya ujenzi wa SILOS (maghala makubwa ya kuhifadhia chakula) pamoja na namna bora ya kuhifadhi chakula, na sisi tuna changamoto ya kuwasadia wakulima kuuza mazao kutokana na uzalishaji mkubwa wa nafaka ambao umetokea mwaka huu,” alisema.
Alisema ni mapema mno kujua kiasi cha fedha ambacho Serikali inatarajia kukopa lakini alithibitisha kwamba atatuma timu ya wataalamu kutoka sekta husika ili wafanye mazungumzo rasmi na Serikali ya Poland na kukamilisha taratibu za upatikanaji wa mkopo huo.
Waziri Mkuu ambaye alisafiri km. 500 kwenda mji wa CHOJNOW kilipo kiwanda cha kutengeneza maghala (SILOS) na kusindika nafaka aliguswa na teknolojia inayotumika kwenye kiwanda hicho cha MLYNPOL ambapo kwa siku moja kina uwezo wa kusindika tani 360,000.
Mji wa CHOJNOW upo kusini Mashariki mwa Poland na pia hauko mbali na mipaka ya nchi za Ujerumani, Czeck na Austria. Kwa gari dogo ni kati ya saa 3 hadi 4 hadi kufika miji mkuu ya nchi hizo ambayo ni Berlin, Prague na Vienna.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, mmiliki wa kiwanda hicho kikubwa nchini Poland, Bw. WITOLD KARCZEWSKI alisema kiwanda hicho kinaposindika ngano kina uwezo wa kutoa unga laini wa mikate (refined flour), unga wa lishe (grain/brown flour), unga wa kutengeneza pasta na tambi na wa mwisho hutolewa kwa ajili ya chakula cha mifugo.
“Nafaka zikifika, zinasafishwa, zinakaushwa, zinapimwa unyevunyevu uliopo na kuanza kusindikwa kulingana na aina ya nafaka inayoletwa. Tunakusanya mazao haya kutoka kwa wakulima kwenye majimbo 16 ya nchi hii,” alisema. Akifafanua kuhusu matumiai ya umeme kwenye kiwanda hicho, Bw. ALEKSANDR ZINGMAN ambaye pia ni mshauri na mbia wa Bw. KARCZEWSKI, alisema kiwanda hicho kinatumia megawati moja ya umeme kwa saa moja lakini matumizi yanaweza kupungua kuligana na ukubwa ama udogo wa kiwanda. “Kama Serikali inahitaji kiwanda kidogo zaidi ya hapa, tunaweza kuwajengea na matumizi ya umeme lazima yatapungua,” alisema.
Kampuni ya MLYNPOL ina wafanyakazi 250 ambao kato yao, 200 wanafanya kazi kiwandani kwa shifti tatu za saa nane nane kila moja.
Nayo KAMPUNI ya URSUS ya kutengeneza matrekta ya kutoka Poland imeonesha nia ya kuja kuwekeza Tanzania na iko tayari kushirikiana na kampuni ya SUMA JKT kutengeneza matrekta hayo. Hayo yamesemwa na Rais wa Bodi ya URSUS, Bw. KAROL ZARAJCZYK wakati akitoa maelezo ya kampuni yake mwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokutana na wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza Tanzania jana asubuhi (Jumapili, Oktoba 26, 2014) kwenye hoteli ya Sheraton jijini Warsaw, Poland.
Bw. ZARAJCZYK alisema wanataka kujenga kiwanda hicho nchini Tanzania kwa kutambua nafasi ya kijiografia ya mahali nchi ilipo kuwa ni fursa ya kufungua milango kwa nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati. “Barani Afrika tulianza kupeleka matrekta Ethiopia, Ghana na Guinea. Sasa hivi tumeamua kuja Tanzania na Zambia. Nia yetu siyo kujenga tu kiwanda bali pia kutoa huduma kwa wakulima juu ya uendeshaji na utunzaji wa hayo matrekta,” alisema.
Alisema wako tayari kutoa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania kama vile chuo fulani ili waweze kuunganisha matrekta hayo hapa nchini na waweze kuyafanyia ukaranati na kutengeneza vipuri vyake pindi ukitokea ulazima wa kufanya hivyo. “Tunapenda kujenga kiwanda mahali ambapo itakuwa rahisi kupata vijana wa kuajiriwa au vijana wa kutoka chuoni ili iwe rahisi kuwafundisha pia teknolojia tunayoitumia kutengeneza matreka hayo,” aliongeza. Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema atawasilisha maelezo yao kwa Waziri anayehusika na sekta hiyo ili mawasiliano rasmi yafanyike.

Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema, atatuma wataalamu wa sekta ya kilimo ili waje kufuatilia suala la mahitaji ya trekta ili kuziba pengo la mahitaji yake nchini Tanzania. Alisema lengo la Serikali la kuanzisha sera ya Kilimo Kwanza lilikuwa ni kuwasaidia wakulima kupata ruzuku ya pembejeo, mbegu bora, na dawa za mifugo ili waweze kuongeza ushalishaji.
“Kutokana na mkopo wa Serikali ya India, tulipata matrekta 1,846 ambayo hayakuchukua muda kuisha. Sasa hivi tunatafuta wabia wengine wa kutupatia zana za kisasa za kilimo kwa sababu matunda yake mazuri tumeyaona, tunataka kilimo cha Mtanzania,” alisema.
Ijumaa, Oktoba 24, 2014), Waziri Mkuu alitembelea kampuni ya Farmers inayotengeneza vipuri pamoja na matrekta ya kulimia na kuvuna yenye ukubwa wa Horse Power 80 na 72 ambayo alielezwa kwamba yanavumilia hali ya udongo mgumu wa Afrika.
Akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Farmer, Bw. ZDZISLAW ZUKIEWICZ alisema vifaa vinavyotengenezwa na kampuni hiyo vina waranti ya miaka saba na vinaweza kuhimili udongo wa miamba na mawe wa ardhi ya Tanzania.
Kampuni hiyo inatengeneza matrekta, mashine za kuvuna mazao shambani (combined harvester), mashine za kukata nyasi za malisho ya mifugo pamoja na vipuri vyake. Alisema bei ya trekta ni wastani wa Euro 22,000 na wako tayari kuleta vifaa hivyo Tanzania kama watapewa oda.
Nao wafanyabiashara wa Poland wameiomba Serikali ya Tanzania kuangalia uwezekano wa kufungua kituo cha biashara katika bara la Ulaya. Wametoa ombi hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kikao kilichowashirikisha wafanyabiashara wakubwa 30 na wamiliki wa makampuni 20 wa hapa Poland kwenye mkutano uliofanyika katika ofisi za Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Poland (Polish Chamber of Commerce) Jijini Warsaw.
Walisema kuwepo kwa kituo hicho barani Ulaya kutawasadia wao kupata taarifa kuhusu Tanzania kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa ambao wanalazimika kwenda London, Uingereza.
Akijibu maombi yao, Waziri Mkuu alisema ombi lao ni la msingi na atawasiliana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe kuona ni nchi gani kituo hicho kinaweza kuwekwa. Kwa upande wake, Kaimu wa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Bw. Christopher Mvula ambaye alimwakilisha Balozi Philip Marmo, alisema ili kituo hicho kiweze kuanza kazi, ni lazima pawe na jengo la ofisi za ubalozi, ofisi za kituo cha biashara na watumishi mahsusi. Balozi wa Ujerumani ndiye anayeiwakilisha Tanzania nchini Poland.
“Lazima kuwe na watumishi wa kituo lakini vilevile kuwe na Afisa Biashara, Afisa Utalii na Afisa Uhamiaji ili kuharakisha baadhi ya mambo. Siyo kila afisa wa ubalozi anaweza kuendesha kituo cha biashara,” alisema. Alisema zitahitajika pia fedha za kulipia matangazo kwenye vyombo vya habari vya nchi husika pamoja na vipeperushi na taarifa nyingine za kuitangaza nchi kupitia kituo hicho.








All the contents on this site are copyrighted ©.