2014-10-27 10:35:00

Ratiba elekezi ya Ibada mbali mbali zitakazoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Novemba 2014


Tarehe Mosi, Novemba, 2014 Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu wote, hawa ndio wale walioshinda mapambano ya maisha ya kiroho kwa kutumainia neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na sasa wametulia mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hii ni siku kuu inayoamsha matumaini makubwa katika maisha ya Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko ataitumia siku hii kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Makaburi ya Roma yaliyoko eneo la Verano, majira ya saa 10: 00 Jioni kwa saa za Ulaya.

Tarehe 2 Novemba 2014, Mama Kanisa anawakumbuka waamini marehemu wote, waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko. Siku hii kwa mara ya kwanza ilianza kuadhimishwa kunako Karne ya tano kwa kuasisiwa na Mtakatifu Odilo, Abate, kwa kukazia umuhimu wa Familia ya Mungu kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu wao. Papa Benedikto wa kumi na tano akaruhusu Mapadre kutolea Misa Takatifu kwa ajili ya kuwaombea Marehemu.

Baba Mtakatifu Francisko, majira ya jioni kuanzia saa 12:00 anatarajiwa kutembelea na hatimaye kusali kwenye Makaburi ya watangulizi wake yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na kusali kwa kitambo kidogo, ili kuwaombea.

Tarehe 3 Novemba 2014, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha Mwaka 2013- 2014.

Tarehe 23 Novemba 2014, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kristo Mfalme wa mbingu na dunia. Huyu ni Mfalme wa milele, ambaye ufalme wake unajengeka katika ukweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, amani na mapendo.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:30 asubuhi kwa saa za Ulaya. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu atawatangaza Wenyeheri wafuatao kuwa ni Watakatifu: Giovanni Antonio Farina; Kuriakose Elias Chavara wa Familia Takatifu, Ludovico da Longobardi, Euphrasia Eluvathingal wa Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na Amato Ronconi.

Kuanzia Ijumaa tarehe 28 hadi Jumapili tarehe 30 Oktoba 2014, Baba Mtakatifu atakuwa na hija ya kiekumene nchini Uturuki kwa mwaliko wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Rais pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Uturuki. Kama kawaida Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakujuza kwa kina na mapana yake yote yatakayojiri katika ratiba hii elekezi. Waswahili wanasema, "chema kula na jirani yako" tafadhali usikose kuwashirikisha jirani zako.







All the contents on this site are copyrighted ©.