2014-10-27 15:20:26

Mwanadamu ni kiini cha maendeleo ya kweli!


Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Jumatatu mara baada ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, mjini Vatican, alitembelea Radio Vatican na kuhojiana na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulinzi na usalama na uhusiano kati ya Serikali na Kanisa nchini Uganda. RealAudioMP3

Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mambo mengine anasema Rais Museveni inapania kuharakisha ustawi, maendeleo, amani na usalama kwa wananchi wa Afrika Mashariki, ili kuweza kupanua soko la mazao ya kilimo na zile zinazozalishwa viwandani na katika sekta ya uvuvi. Kwa njia hii, watu wataweza kuendelea zaidi kutokana na kupanuka kwa soko la bidhaa.

Rais Museveni anasema kwamba, wataalam wa masuala ya fedha na uchumi kwa sasa wanaendelea kushughulikia uundwaji wa sarafu ya pamoja miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, kwanza kwa kuweka uwiano na mwingiliano wa sera. Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki tayari wamekwisha ridhia kuanzishwa kwa sarafu moja, sasa wanaendelea kukamilisha utekelezaji wake kwa wakati muafaka.

Rais Museveni anasema amani, usalama na utulivu ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga na wananchi wenyewe kwa kutambua kwamba, ulinzi na usalama uko mikononi mwa wananchi wenyewe. Hata hivyo anakumbusha kwamba, vita ni matokeo ya siasa chafu, ubinafsi, umaskini na ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana.

Ili kudumisha amani kuna haja kwa nchi mbali mbali duniani kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, kuimarisha siasa safi; kusimamia ulinzi na usalama kwa kuwa na miundo mbinu makini pamoja na kupembua sera ambazo zitasaidia kupambana na umaskini na ukosefu wa fursa za ajira. Hii ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na Serikali pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo.

Rais Museveni amesema kwamba, amemwalika rasmi Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Uganda, lakini bila kufafanua zaidi kwa kusema kwamba, "hii ni siri ya wazee hawa". Anasema ameguswa na jitihada za Baba Mtakatifu katika kutetea haki msingi za binadamu hasa wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na mifumo ya uchumi kimataifa inayojikita katika faida kubwa bila ya kujali maendeleo endelevu ya binadamu. Binadamu anapaswa kuwa ni kitovu cha maendeleo na wala si fedha au faida kubwa. Serikali na dini zinaweza kushirikiana vyema zaidi katika kuharakisha mchakato wa maendeleo endelevu.

Rais Museveni amewataka wananchi Barani Afrika kujikita katika ujenzi wa misingi ya umoja na uzalendo; upendo na mshikamano wa dhati kwa kupinga kwa nguvu zote ukabila na udini, sumu kali ya maendeleo ya watu. Mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya maendeleo, ili kukuza na kujenga Bara la Afrika linalocharuka katika maendeleo si tu ya vitu bali ya watu.







All the contents on this site are copyrighted ©.