Maneno yetu yanaweza kutangaza iwapo sisi ni Wakristo wa kweli , au ni watu wa giza
au ni Wakristo nusunusu.
Ni muhimu kuchunguza dhamiri ya maneno au lugha
tunayotumia katika mazungumzo kwa kuwa huonyesha hadhi na imani ya mtu, iwapo ni
mtoto wa mwanga wa kweli wa Kristo , au ni mtoto wa shetani au iwapo Ukristo wetu
upo nusunusu, Baba Mtakatifu Francisko alieleza katika hotuba yake mapema Asubuhi
katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta.
Maelezo ya Papa, yalilenga katika
somo kutoka barua ya Mtume Paulo kwa Waefeso , ambamo mnasema, watu huweza kutambuliwa
kwa maneno yao. Papa alirejea barua hiyo na kutoa mwaliko kwa Wakristo, kutenda na
kuzungumza na kuishi kama watoto wa mwanga, na si kama watoto wa giza. Maneno ya
Mtume Paulo ni mafundisho ya kina, ambamo ndani mwake kuna maneno yanayoweza kutuonyesha
iwapo sisi ni watoto wa giza.
Papa alieleza na kuhimiza kila mmoja kujihoji
iwapo tunazungumza kinafiki kwa lengo la kuchota kidogo hapa, na pia kidogo kule na
kuwa mtu wa katikati, mnafiki mchonganishi, asiyeeleweka, anasimama upande gani. Papa
alihoji kuwa mtu wa aina hiyo kumfaa nini mtu? Aliitaja tabia hiyo kuwa ni unafiki
mtupu. Alindelea kukemea mazoea ya kutoa matusi na kudhihaki wengine, kuwa na maneno
yasiyo faa, maneno yasiyokuwa na maana yenye kusababisha migogoro hata kwa mambo
madogomadogo yasiyokuwa na maana,. Lugha Chafu, daima haijengi bali huboa na ni ubatili
mtupu na upuuzi mtupu.
Papa amesema, lugha chafu si lugha ya watoto wa
mwanga , wala si kutoka kwa Roho Mtakatifu, na wala si kutoka Yesu, watu hao si wana
wa Injili ... njia hiyo ya kuzungumza, daima juu ya mambo machafu huongoza katika
kuyapenda ya dunia na mambo yake ya kibatili na unafiki.
Basi, ni yapi
maneno ya Watakatifu, au ya watoto wa mwanga wa Kristo?
Papa Francisko alitoa
ufafanuzi kwa kurejea barua za Mtakatifu Paulo ambamo anasema, Igeni Mungu, kutembea
katika upendo, kutembea katika wema, kutembea katika upole, kwa kuwa wale wanaotembea
katika njia hii ....hujaliwa neema ya huruma. Mtume Paulo anasema, kusameheana kama
Mungu alivyowasamehe ninyi pia katika Kristo. Basi, wafuasi wa Mungu hutembea katika
upendo , yaani, kutembea katika huruma, msamaha na upendo.Hayo ndiyo maneno ya mtoto
wa mwanga. Hao ni Wakristo thabiti walio katika mwanga kamili, alibainisha Papa -
ambao wanataka kumtumikia Bwana katika mwanga huu.
Papa pia alieleza juu
ya kundi jingine kundi la Wakristo wanaoishi katika giza, ambao maisha yao yanaongoza
katika kutenda dhambi, maisha ya kuwa mbali na Bwana na ambao lugha yao huwaonyesha
kuwa mbali na Kristo. Watu waliojitenga na kanisa na kuyakumbatia ya dunia hii.
Aidha
Papa, alizungumzia kundi la tatu la Wakristo", ambao si mwanga wala giza, akiwataja
kuwa wao ni Wakristo walio katikati, maisha yao hayajulikani wako kundi gani, iwapo
ni Wakristo au la. Hawa ni Wakristo wa rangi ya kijivu si nyeupe wala nyeusi wako
tu hapo, haijulikani kama ni watu wa Mungu au ni wafuasi wa shetani. Papa alionya
kwamba, Mungu hapendi watu wa aina hiyo. Watu wasiokuwa na maamuzi thabiti katika
maisha. Alieleza kwa kurejea kaitkakitabu cha Ufunuo,ambamo Bwana anasema, kwa kuwa
wewe ni si moto wala baridi nitakutapika kutoka kinywa changu .. Ni maneno ya kutisha
kutoka kwa Bwana, kwa ajili ya Wakristo hao walio katika eneo la uvuguvugu, wenye
kusema Mimi ni Mkristo, lakini hawaonyeshi lolote katika Ukristo wao . Maneno na
vitendo vyao huwa na madhara makubwa, kwa sababu ushahidi wao kama Wakristo huishia
kupanda mbegu isiyoeleweka , na mara nyingi hupandikiza fujo na ushahidi hasi.
Papa
alihitimisha homilia yake kwa kuhimiza kuishi kama watoto wa mwanga. Na kwamba, watu
wote inafaa kutafakari vyema, iwapo maneno na matendo yetu, yanatoa miali ya mwanga
wa mwanga wa Kristo, au iwapo tu wakristo wa giza?au tu Wakristo wa uvuguvugu, tusiojulikana
tuko wapo, Mkristo wa katikati?
Papa ametoa mwaliko kwa watu wote, kuchukua
hatua za mbele katika kuwa na mwanga wa kukutana na Bwana.