2014-10-27 08:33:01

China kuendeleza eneo la kiuchumi Bagamoyo!


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi mbili kubwa za kimataifa Jumapili, Oktoba 26, 2014, zilitiliana saini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kuendeleza kwa pamoja Eneo la Kiuchumi la Bagamoyo ambako pia itajengwa bandari kubwa ya Bagamoyo ambayo inatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa Tanzania.

Pande hizo tatu ambazo ni pamoja na Kampuni ya Uendeshaji Bandari ya China Merchant Holding International (CMHI) ya Jamhuri ya Watu wa China na Mfuko wa Uwekezaji wa Oman wa State General Reserve Fund of Oman ya Oman zimetilia saini Hati hiyo kwenye sherehe iliyofanyika katika Hoteli ya Hilton Shenzhen Shekou Nahai ya mjini Shenzhen, Kusini mwa China.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ametembelea Jimbo la Guang Dong ambako liko Eneo la Uwekezaji wa Kiuchumi la Shenzhen alishuhudia utiaji saini huo ambao kwa upande wa Tanzania saini ilitiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Servicus Likwelile. Chini ya Hati hiyo ya uendelezaji wa Eneo la Uwekezaji la Bagamoyo litaanza kujengwa Julai Mosi mwakani, 2015.

Kabla ya sherehe hiyo ya kutiliana saini Hati ya Makubaliano, Rais Kikwete ametembelea Eneo la Kontena la Bandari ya Shenzhen ambako alionyeshwa vifaa vya kisasa kabisa vya kupakia na kupakulia kontena kazi inayofanywa na CMHI ambayo ina uzoefu wa miaka 140 wa uendeshaji wa bandari.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake imedhamiria kuhakikisha kuwa mradi huo wa mamilioni ya fedha wa Bangamoyo unaanza. “Tutafanya lolote linalowezekana kuhakikisha kuwa mradi huu unaanza kwa sababu utaleta neema kubwa ya kiuchumi kwa nchi nzima.”

Naye Mwenyekiti wa CMHI, Bwana Li Jianhong ameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kumaliza vikwazo vyote ambavyo vimechelewesha kuanzishwa kwa mradi huo ili uweze kuanza Julai Mosi, mwakani, kama ilivyokubaliwa.

Mapema siku ya Jumapili akiwa Shenzhen, Rais Kikwete ametembelea makao makuu ya Kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya Hauwei Technologies inayoajiri maelfu ya watu duniani, ikiwemo Tanzania, na kutengeneza mamilioni ya faida. Aidha, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Manispaa ya Shenzhen ambayo yalifanyika kwenye hoteli ambako alifikia Rais Kikwete katika ziara yake ya Shenzhen ya Shenzhen Wazhou Guest Hotel ambayo ni mali ya Serikali ya China.
Rais pia ametembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Teknolojia ya Mawasiliano ya ZTE iliyoko mjini Shenzhen ambayo inaendesha shughuli zake Tanzania na inaajiri wafanyakazi 60,000 dunia nzima.

JK Rais wa kwanza kupokelewa kwa pikipiki China kwa miaka 10 iliyopita!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesababisha mageuzi makubwa kwa namna Jamhuri ya Watu wa China inavyowapokea viongozi wageni kutoka nje kwa kuwa kiongozi wa kwanza duniani kupokewa rasmi na pikipiki za Polisi na kuongozwa na pikipiki hizo kwa muda wote wa ziara katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Rais Kikwete ambaye aliwasili nchini China Jumanne iliyopita, Oktoba 21, 2014, kuanza ziara rasmi ya siku sita nchini humo, amekuwa kiongozi wa kwanza wa nje kupokelewa na msafara wa pikipiki tokea Januari Mosi, mwaka 2004, miaka 10 iliyopita wakati China ilipofuta utaratibu wa misafara ya viongozi kusindikizwa na pikipiki za Polisi.

Rais Kikwete na msafara wake alipokewa na msafara wa pikipiki wa polisi mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Beijing hadi kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya Diaoyutai, katikati ya Jiji la Beijing na utaratibu huo kuendelea kuongoza msafara wake kwa siku zote alipokuwa China. Taarifa ya habari iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya China na kukaririwa na Shirika la Habari la nchi hiyo la Xinhua haikutoa sababu zozote za mabadiliko ya sera hiyo.

Katika nchi karibu zote duniani, utaratibu wa viongozi wa nchi mbali mbali kupokelewa kwa misafara ya pikipiki ni protokali ya juu kabisa ambayo pia huongeza usalama wa kiongozi na ni utaratibu wa kawaida katika nchi nyingi duniani. Tokea kuasisiwa kwake mwaka 1949, Jamhuri ya Watu wa China ilikuwa na utaratibu wa pikipiki za polisi kuongoza misafara ya viongozi lakini utaratibu huo ulisimamishwa Januari Mosi, mwaka 2004, kwa sababu ambazo hazijapata kuelezwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.