2014-10-25 14:52:46

Vijana msikate tamaa niko pamoja nanyi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Oktoba linaadhimisha Kongamano la Vijana Kitaifa huko Salerno, Kusini mwa Italia linaloongozwa na kauli mbiu "Matumaini katika hali ya ukosefu wa ajira". Lengo la Kongamano hili ni kuwajengea tena vijana matumaini, hasa wakati huu wanapokabiliana na changamoto mbali mbali na mabadiliko makubwa katika maisha ya vijana wa kizazi kipya.

Hiki ni kipindi ambacho vijana wengi wanakabiliwa na wasi wasi, hali ya kukosa mwelekeo na dira ya maisha pamoja na mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe vijana wanaoshiriki katika kongamano hili kwa kuwashirikisha uzoefu na mang'amuzi yake wakati anapofanya hija za kichungaji nchini Italia. Anasema, katika hija hizi zote amebahatika kukutana uso kwa uso na na hali ya vijana wengi ambao hawana fursa za ajira au wako katika mpango wa kuachishwa kazi. Hili si tu kwamba, ni tatizo la kiuchumi bali pia ni hali inayogusa utu na heshima ya binadamu anayejisikia kuwa mnyonge kiasi hata cha kushindwa kupata mahitaji msingi.

Baba Mtakatifu anasema mahali ambapo hakuna fursa za ajira hapo utu wa mtu uko mashakani na kwamba, inasikitisha kuona kuwa Italia kuna vijana wengi wa kizazi kipya hawana fursa za ajira, zinazowahakikishia usalama na matumaini kwa ajili ya maisha ya kesho iliyo bora zaidi sanjari na kujiwekea mikakati ya kuanzisha na hatimaye kujenga familia.

Nyakati hizi vijana wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha, kiasi kwamba, utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine unaanza kushika kasi ya ajabu, kwani pale ambapo hakuna faida, utu na heshima ya binadamu vinawekwa rehani. Mwelekeo kama huu ni hatari kwa maisha ya vijana wa kizazi kipya, changamoto kwa Jamii kusimama kidete kupinga utamaduni wa kutojali mahangaiko ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, licha ya mahangaiko na mateso wanayokabiliana nayo vijana katika maisha yao, kuna neno la matumaini, mwaliko kwa vijana kutokubali kamwe baadhi ya watu kuwapokonya matumaini yao, bali waendelee kujikita katika nguvu ya Injili, chemchemi ya matumaini kwani inabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa Mwanaye wa Pekee, Yesu Kristo aliyefanyika Mwili, ili kujishikamanisha na binadamu.

Vijana wanakumbushwa kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa; wana zawadi na dhamana ya kutekeleza kwa njia ya mwanga wa Injili katika maisha ya kijamii na kitamaduni. Injili ni chimbuko la watu kukutana ili kujenga mshikamano wa kidugu, changamaoto kwa vijana kuwa ni kielelezo cha matumaini hata katika hali ya ukosefu wa fursa za ajira.







All the contents on this site are copyrighted ©.