2014-10-25 14:57:30

Jubilee ya Miaka Karne Moja tangu kuanzishwa kwa Chama cha Schoenstatt


Sisi ni Kanisa linalosafiri duniani ndiyo kauli mbiu iliyooongoza maadhimisho ya Jubilee ya Karne moja tangu kuanzishwa kwa chama cha kitume cha Schoenstatt na kuhudhuriwa na wanachama elfu saba kutoka katika nchi hamsini duniani, ambao siku ya Jumamosi tarehe 25 Oktoba 2014 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, mjini Vatican ili kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa karama hii muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Chama hiki kilianzishwa na Padre Josef Kentenich, tukio ambalo limehudhuriwa pia na viongozi waandamizi kutoka ndani na nje ya Vatican. Tasaufi ya chama hiki inajikita katika upendo unaofumbatwa katika agano na Bikira Maria na kwamba, Jubilee ya miaka mia moja ni mwaliko wa kurudi tena kwenye mizizi ya maisha yao ya kiroho kwa kuonesha upendo kwa Bikira Maria ambao umemwilishwa katika nchi mbali mbali duniani na kwa upande wa Bara la Afrika, upendo huu umejionesha kwa namna ya pekee nchini Burundi.

Ibada ya Neno la Mungu imeongoza maadhimisho ya Jubilee ya Miaka mia moja ya Chama cha Schoenstatt pamoja na kufanya majadiliano ya kina na Baba Mtakatifu Francisko, ili kukazia umuhimu wa familia kama kiini cha maisha ya mwanadamu; changamoto katika malezi na makuzi ya watoto, mwaliko kwa familia kumuiga Bikira Maria wakati wanapotekeleza wajibu wao.

VIjana wanachangamotishwa na Mama Kanisa kujitosa kimasomaso katika mchakato wa maisha na utume wa Kimissionari, huku Waamini wakijitahidi kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa ndani ya Jamii, lengo likiwa ni kuyatakatifuza malimwengu. Wanachama hawa wamejiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na katika Jamii kwa ujumla.







All the contents on this site are copyrighted ©.