2014-10-24 12:32:00

Zambia inaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wake kwa kupata Rasimu ya Katiba Mpya!


Jukwaa la Wakristo nchini Zambia linaloungayaunganisha Mabaraza mbali mbali ya Makanisa nchini Zambia, katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Zambia ilipojitwalia uhuru wake kutoka kwa Mwingireza hapo tarehe 24 Oktoba 1964, limeandika ujumbe unaowapongeza wananchi wa Zambia kwa kuendelea kudumisha amani na umoja wa kitaifa, licha ya misukosuko mbali mbali iliyojitokeza nchini humo katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Jubilee ni kipindi cha kumshukuru Mungu na kufanya tafakari ya kina kuhusu mapungufu ili kuweza kuyarekebisha kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi wa Zambia kwa siku za usoni. Kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita, Serikali na Kanisa kwa pamoja wameshikamana katika kuwahudumia wananchi wa Zambia katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Ni matumaini ya Jukwaa la Wakristo kwamba, kwa pamoja wataendelea kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.

Zambia imeonesha maendeleo kidogo katika masuala ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa; nchi imeendelea kuwa ni makazi ya wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanatafuta hifadhi na usalama wa maisha yao na kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ingawa changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na mgawanyo bora zaidi wa huduma na raslimali ya nchi ya Zambia kwa watu wake wote, ili maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Rasilimali ya nchi haina budi kutumika kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa na utawala bora, mambo ambayo bado yanapaswa kufanyiwa kazi kwa siku za usoni. Zambia imeendelea kubeba mzigo wa deni kubwa la ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, zigo linalowaelemea wananchi wa Zambia, changamoto ya kuwa na matumizi bora na sahihi ya fedha za umma, sera na utekelezaji makini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Zambia.

Zambia kwa siku za usoni, haina budi kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki jamii, mafao ya wengi na sera za maendeleo endelevu kwa wananchi wote, kwa kujikita katika misingi ya upendo, ukweli, umoja, ukarimu, uwajibikaji na mshikamano wa dhati, ili kweli Zambia iweze kuwa ni nchi moja si tu kwa maneno bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Umaskini unaendelea kuwaelemea wananchi wengi wa Zambia wanaoishi mijini, lakini zaidi wale wanaoishi vijijini, changamoto kwa Serikali na wadau mbali mbali kujifunga kibwebwe kupambana na umaskini.

Zambia inaadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wake, ikimshukuru Mungu kwa kupata Rasimu ya Katiba Mpya, ambayo imewatesa sana wananchi wa Zambia kiasi hata cha kutishia usalama, umoja, mshikamano na mustakabali wa wananchi wa Zambia. NI matumaini ya Jukwaa la Wakristo kwamba, Serikali ya Zambia itaonesha ratiba ya mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Zambia.

Wananchi waelimishwe umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii, huku wakidumisha: haki na amani. Mashirika ya misaada yatumie fursa na rasilimali zake katika kupambana na umaskini nchini Zambia. Wanavishukuru vyombo vya habari nchini Zambia kwa kusaidia kuwahabarisha wananchi wa Zambia.

Ujumbe huu umehaririwa na
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.