2014-10-24 08:07:58

Hapa ni bifu tupu hadi kieleweke!


Katika wiki ya mwisho ya maisha yake hapa duniani, Yesu alipambana na mizengwe mingi sana na kuchafuana nyongo na wafarisayo, masadukayo, waherode nk. Watu hao wakamkabili Yesu kwa maswali ya kebehi na ya mtego ili mradi wapate mwanya wa kumshika na kumshtaki apate kuuawa. Yasemwa kwamba kulikuwa na “migogoro mitano ya Yerusalemu” dhidi ya Yesu: Mgogoro wa kwanza, ulihoji mamlaka yake; mgogoro wa pili ni wa kiuchumi na kisiasa, yaani uliohusu kulipa kodi kwa Kaisari; mgogoro wa tatu, ulihoji suala la ufufuko; mgogoro wa nne ulihoji amri iliyo kuu; na mgogoro wa tano ulihoji suala la umasiha wa Yesu mwana wa Daudi.

Ukiangalia kwa makini utagundua pia kwamb,a wale waliokuwa wanamwandama na kumhoji Yesu hawakuwa raia wa kawaida, bali walikuwa watu wa ngazi za juu katika serikali na dini. Yaani, walikuwa viongozi, wataalamu na wasomi wa hali ya juu kama vile wanasheria wakuu wa nchi, majalimu nk. Aidha walikuwa wamejipanga kwa hoja nzito ili kumtafuta ubaya. Kwa bahati nzuri hata Yesu mwenyewe alishawaelewa na alishajua kuwa ufalme wake ulikuwa unakataliwa na baadhi ya watu hasa na wale waliojidai kuwa wanaelewa kila kitu.

Lakini kwa vile hakutaka kuingilia uhuru wa mtu akaacha kila mmoja achague anavyotaka mwenyewe. Yeye kwa upande wake akawa tu anawahubiria na kuwaonya watu wote bila kujali cheo au dini ya mtu, akianza kuwakosoa viongozi wa serikali na raia wao na wakati mwingine akiwaangalisha kwa lugha kali hasa pale alipoikemea miji yao “ole wako Korazini, ole wako Betsaida…” nk. Kadhalika hakuwakopesha viongozi wa dini bali anawalipua waziwazi alipowaambia: “ole wenu mafarisayo na wakuu wa makuhani” nk.

Leo Yesu anapambana na mgogoro wa nne wa Yerusalemu, yaani anapohojiwa juu ya amri kuu. Ndipo anapolipuana na wataalamu na wakuu wa dini. Wataalamu hao walimjia Yesu wakiwa wamejipanga kwa lugha tunayoweza kusema ya kidiplomasia. Wanamwuliza Yesu swali linaloeleweka hata na mtoto mdogo. Kwa hiyo yatubidi hata sisi kuwa mahili sana ili kuweza kuuona mtego uliojificha katika swali hilo, hadi tuweze kupata fundisho kwa siku ya leo.

Kwanza kabisa Wafarisayo wanaofika kwa Yesu walikuwa wamesikia kwamba Yesu amewafumba vinywa Wasadukayo. Kama mjuavyo, Wafarisayo na Wasadukayo walikuwa na sera na itikadi tofauti za kisiasa, za kiserikali hata kidini, nk. Kama ilivyokuwa kwa waherodi, Wasadukayo walikuwa matajiri, walikuwa wanaendesha liturjia katika mahekalu, wanachagua kondoo walionona na wenye sufu safi wa kutolewa sadaka hekaluni.

Walikuwa wanawaenzi sana watu matajiri, lakini pia walikuwa hawasadiki kabisa juu ya malaika, au juu ya maisha baada ya kifo, wao hawakuamini juu ya paradisi yaani ufufuko isipokuwa waliamini maisha ya hapa duniani tu. Yesu aliwafumba midomo watu hao alipowajibu swali juu ya yule mwanamke aliyekuwa na wanaume saba, kwamba ni mwanaume gani angekuwa mume wake kwenye ulimwengu wa ufufuko.

Kumbe Wafarisayo waliamini juu ya ufufuko, kama alivyosadiki Marta, aliyemwambia Yesu kuwa ninasadiki kwamba wafu watafufuka. Aidha kifikra za kiteolojia wafarisayo walikuwa karibu zaidi na Yesu kwani walikuwa wafuatiliaji wazuri wa Maandiko Matakatifu, isipokuwa tafsiri waliyokuwa wanaitoa ilitofautiana na ile aliyokuwa anaitoa Yesu. Wakati huo Yesu alishachafuana pia na wafarisayo pale alipoingia Yerusalemu na kuwaharibia biashara zao hekaluni. Hata kabla yake alikuwa amewaudhi alipowakosoa juu ya matumizi potovu ya tora ya kutojali utu wa mtu, na kuita mali hiyo kuwa ni korbani. Sasa Wafarisayo hao wanatafuta mwanya wa kumbambikizia ubaya.

Kabla ya kumwendea wanaungana pamoja ili kupanga mikakati ya jinsi ya kumwingia. Wakamchagua mtaalamu wao mmoja wa Teolojia na Maandiko matakatifu na mwana-sheria aliyebobea ili awe msemaji wao. Akamwuliza: “Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?” Angalia hapa, hawaulizi kuwa ipi ni amri iliyo kuu zaidi katika torati. Swali hili ni rahisi kabisa na wayahudi wote hadi watoto wadogo walilifahamu jibu lake, kwamba kuna amri kuu moja tu nayo ni ya kumpenda na kumwabudu Mungu mmoja. Amri hiyo walikuwa wanaishika wote siku ya sabato.

Kwa nini basi wamwulize Yesu swali jepesi walilokuwa wanalifahamu. Kwa kweli Rabi huyu anapouliza swali hilo, hakuhitaji jibu, bali alichotaka kusema ni kama kumwuliza Yesu “kwa nini wewe hushiki amri hiyo ya sabato?” Yesu hawezi kumjibu mtaalamu huyo kwa jibu hilo, kwa sababu kama mmoja ameshafungwa na mapokeo yake, ameng’ang’ana na mfumo wake wa mawazo, akili yake imeganda hivyo, na ameridhika na hali. Katika kulijibu swali hilo Yesu hanukuu amri yoyote ile bali anasema: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote ,na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.” Yesu anasema kwa akili zako zote na kwa roho yako yote.

Kwa roho yako yote. Kwamba kila maamuzi yaanze na kile anachotaka Mungu. Mungu peke yake aongoze maisha. Mungu awe katika mawazo yote (akili). Imani kwa Mungu lazima iwe tunda la maamuzi yote ya Mungu (roho).

Amri ya pili ni sawa na hiyo, ambayo Yesu anachukua toka kitabu cha walawi yaani kumpenda jirani kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Bila kupenda hivyo huwezi ukaifuata kikamilifu ile amri ya kwanza. Akaongeza kusema kuwa amri hizi zimeegemezwa katika manabii na torati.

Amri hizi mbili zinatoa fursa kwa Mungu na binadamu. Amri zote mbili ni sawa, yaani ni amri moja tu siyo mbili. Ukimpenda Mungu maana yake ni kumpenda jirani. Ukimpenda jirani utakuwa hivyo umempenda Mungu. Baada ya jibu hilo, Yesu hakupata tena swali jingine, ikawa kama vile nao amewafumba midomo.

Jambo tunaloweza kujifunza hapa ni kwamba, wakati mwingine tunakuwa na majibu yetu tayari, yaani tunang’ang’ana na fikra zetu, tukijidhania kwamba ni jambo linalojukana kumbe hatujui kwamba tumeshapotoka na fikra hizo. Daima tufumbue akili zetu kwa Kristu, kwani Yeye ni jibu pekee.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.