Jitoeni kimasomaso kuonesha upendo kwa Mungu na jirani!
Roho Mtakatifu anawawezesha Wakristo kupata nguvu ya kupenda na kujitosa kimasomaso
bila ya kujibakiza kama alivyofanya Mtakatifu Paulo katika barua yake kwa Waefeso,
kwa kuwashirikisha uzoefu na mang'amuzi ambayo yalimfanya kuacha yote, kwa vile alitaka
kuonesha upendo wa dhati kabisa kwa Kristo.
Hiki ni kielelezo makini cha mtu
anaye abudu kwa kumpigia Mwenyezi Mungu magoti, kwa kutambua kwamba, ana uwezo wa
kufanya mambo mengi hata yale ambayo mwanadamu athubutu kuomba mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hayo
yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anatoa mahubiri kwenye Ibada
ya Misa Takatifu, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Siku
ya Alhamisi asubuhi tarehe 23 Oktoba 2014
Mtakatifu Paulo anawaalika waamini
kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumpenda bila kikomo na anawaombea ili kweli waweze kuimarishwa
katika utu wao wa ndani kwa njia ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anawaimarisha waamini
na kuwapatia nguvu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini, kwa kutambua kwamba, kutokana
na unyonge wao wa kibinadamu, wakati mwingine wanakosa nguvu na ujasiri. Ni kwa njia
ya neema ya Roho Mtakatifu watu wanawezeshwa kuwa ni Wakristo, tayari kusonga mbele
katika utekelezaji wa Amri za Mungu.
Mtakatifu Paulo anawaombea Wakristo neema
na baraka kutoka kwa Yesu Kristo, ili awawezeshe kukua na kukomaa katika upendo wa
Kristo usiokuwa na mipaka, unaoonesha ukuu wa Mungu. Haya ndiyo mang'amuzi ya Mtakatifu
Paulo kuhusu: Sala ya kusifu na kuabudu dhidi ya mapungufu yanayoweza kujitokeza kwa
waamini wakati wa sala. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kusonga mbele kwa kufarijika
na kujizamisha katika upendo unaobubujika kutoka kwa Yesu Kristo.
Baba Mtakatifu
Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, huu ndio msingi wa maisha
ya kiroho, unaomwezesha mwamini kutambua jinsi ambavyo Mtakatifu Paulo alivyoacha
yote, ili aweze kumpata Kristo na baadaye kupata yote ndani ya Kristo. Ni ajabu ya
kupendeza kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu, kwa kuwagawia wengine upendo na ukarimu
unaobubujika kutoka kwa Yesu Kristo. Kwa njia hii, waamini wanaweza kusonga mbele
katika mchakato wa kumwilisha ile Amri kuu ya mapendo kwa Mungu na jirani.