Endeleeni kusali na kuchangia mawazo kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Familia
kwa Mwaka 2015
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, wakati wa maadhimisho ya Sinodi
Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia iliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe
5 ahdi tarehe 19 Oktoba 2014, ilikuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kusikiliza kwa makini
ushuhuda na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume
wa Familia. Kanisa limemwangalia Kristo, ili liendelee kutangaza Injili ya Familia
kwa Watu wa Mataifa, huku likikabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na
utume wa Familia.
Askofu Ngalalekumtwa
ambaye alikuwa analiwakilisha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho
ya Sinodi hii anasema kwamba, awamu ya kwanza imehitimishwa na hati ya Mababa wa Sinodi
itakuwa ni mwongozo na rejea katika kujiaandaa kwa ajili ya maadhimisho ya awamu ya
pili ya Sinodi itakayofanyika kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuongozwa
na kauli mbiu "Wito na utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo". Mababa
wa Sinodi wametafakari kwa kina na mapana baraka ya maisha ya ndoa na familia kadiri
ya mpango wa Mungu.
Askofu Ngalalekumtwa anasema wanandoa watarajiwa wanahaki
ya kuandaliwa vyema ili waweze kutambua dhamana na utume wao katika Kanisa. Wanapofunga
ndoa, wasindikizwe kwa hekima na busara, ili kuendelea kupyaisha upendo wa maisha
ya ndoa na familia. Wanandoa wanapaswa kujiandaa kikamilifu: kiakili, kiroho na kijamii
ili kuipokea Sakramenti ya Ndoa kwa imani na matumaini na hatimaye kufurahia baraka
ya ndoa.
Askofu Ngalalekumtwa anasema, kwa hakika ndoa inahitaji malezi endelevu,
ili kuimarisha kifungu cha upendo na mshikamano wa dhati. Kinzani, migogoro na hatimaye
talaka ni dalili za kuanza kuporomoka ile neema ya maisha ya ndoa na familia. Wanandoa
wanakumbushwa kwamba, wao ni kielelezo cha upendo wa Kristo kwa Kanisa lake. Kristo
anaendelea kulipenda Kanisa licha ya mapungufu yanayofanywa na watoto wake.
Tangu
sasa waamini waendelee kusali kwa ajili ya Sinodi, wakitafakari na kuchangia mawazo
kuanzia katika familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Vigango, Parokia, Majimbo
hadi ngazi ya kitaifa na kikanda, ili Kanisa liweze kutambua matatizo, changamoto
na fursa zilizopo kama sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa
Injili ya Familia. Kanisa linawahitaji watu wenye msimamo thabiti katika maisha na
kwamba, mchango wa waamini utawawezesha Mababa wa Kanisa kutambua makali yanayozikabili
familia!