2014-10-22 09:09:48

Vatican inafuatilia kwa makini hali ilivyo huko Mashariki ya Kati!


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akichangia mada kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni anasema kwamba, Vatican inaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi hali ya mashariki ya Kati pamoja na majadiliano ya kisiasa kuhusiana na mgogoro kati ya Israeli na Palestina pamoja na kuendelea kukazia umuhimu wa pande zinazohusika kujikita katika majadiliano ili amani, utulivu na maendeleo viweze kupatikana.

Kutokana na kuguswa na mahangaiko ya watu huko Mashariki ya Kati, hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko amefanya mikutano kadhaa ili kuangalia jinsi ambavyo Kanisa linaweza kusaidia kuharakisha upatikanaji wa suluhu ya kudumu huko Mashariki ya Kati kwa kuzingatia sheria za kimataifa, haki msingi za binadamu na mshikamano wa kidugu.

Ujumbe wa Vatican unaunga mkono uwepo wa Mataifa mawili ya Israeli na Palestina, kazi inayopaswa kushughilikiwa na Umoja wa Mataifa, huku ukiungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa. Lengo ni kuwawezesha Wapalestina kuwa ni taifa huru linalojitegemea na kujiamria mambo yake lenyewe, kwa kutambua mipaka yake na haki ya kuwepo kama taifa, ili amani na utulivu viweze kudumishwa.

Kuna uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu nchini Syria, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwasaidia wananchi wa Syria, ili amani na utulivu viweze kurejea tena na kwamba, Lebanon ni mfano wa kuigwa kwa watu kuishi kwa amani na utulivu, huku wakiheshimiana na kuthaminiana. Umoja wa Mataifa hauna budi kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia mauaji ya kimbari huko Iraq na Syria, pamoja na kutoa ulinzi wa kutosha kwa wakimbizi wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao.

Ujumbe wa Vatican unaendelea kuwahimiza viongozi wa kidini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuhakikisha kwamba, wanasaidia kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kwa kupinga wale wanaofanya mauaji kwa kisingizio cha udini. Watu wafahamiane, waheshimiane na kusaidiana kutafuta mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusaidia harakati za amani na utulivu huko Mashariki ya Kati, kwani hali inazidi kuwa mbaya kila kukicha!







All the contents on this site are copyrighted ©.