Simameni kidete kulinda na kutetea haki za watoto duniani
Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa
anasema kwamba, hivi karibuni, Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF
limeonesha kwa kina na mapana juu ya upembuzi yakinifu wa matatizo na changamoto zinazowakabili
watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kubainisha
mikakati itakayotumika kuwalinda na kuwaendeleza watoto, ili kupunguza vifo vya watoto
wadogo.
Ili kufikia lengo hili kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea
kuwekeza katika lishe bora, maji safi na salama pamoja na uhakika wa elimu bora na
wala si bora elimu.
UNICEF katika taarifa yake inaonesha kwamba, kuna kundi
kubwa la watoto linaloendelea kunyanyasika na kudhulumiwa kwa kutumbukizwa kwenye
biashara haramu ya binadamu, ngono na picha chafu. Katika miaka ya hivi karibuni,
takwimu zinaonesha kwamba, kuna watoto zaidi ya millioni tatu wamefariki dunia katika
vita na kinzani za kijamii; watoto millioni sita wamepata umelevu wa kudumu na wengine
kujeruhiwa vibaya kutokana na milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini na kwamba, licha
ya kampeni ya kimataifa, lakini bado kuna watoto ambao wanalazimishwa kwenda mstari
wa mbele, na wengine siku hizi wanatumika katika mashambulizi ya kujitolea mhanga;
mambo ya kusikitisha sana!
Askofu mkuu Auza anasema, kuna kundi kubwa la watoto
ambao wamefariki dunia kutokana na sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo; kuna watoto
wanateseka kutokana na utapiamlo wa kutisha, ukosefu wa makazi na dawa msingi na matokeo
yake, watoto hawa wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na mambo yanayo
wanyanyasa na kudhalilisha utu na heshima yao. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa
na Serikali husika kuhakikisha kwamba, zinazijengea familia uwezo wa kutekeleza dhamana
na wajibu wake, hasa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapofanya kumbu kumbu ya miaka
ishirini tangu Mwaka wa Familia Kimataifa ulipoadhimishwa kwa mara ya kwanza.
Wazazi
na watoto wafundishwe faida na madhara ya kutumia mitandao ya kijamii; wazazi watekeleze
dhamana ya malezi na makuzi kwa ukamilifu zaidi, ili watoto hawa waweze kuwa ni raia
wema na wanaowajibika barabara katika ustawi na maendeleo ya Jamii zao.
Askofu
mkuu Auza anasema kwamba, Mwezi Novemba, 2014 Jumuiya ya Kimataifa itaadhimisha Kumbu
kumbu ya miaka 25 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa
kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima
yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi
na maendeleo yao kiroho na kimwili.
Itakumbukwa kwamba, Kanisa limekuwa mstari
wa mbele katika kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa
kuwapatia chakula, makazi, malazi, elimu na huduma ya afya. Kanisa litaendelea kutekeleza
wajibu huu msingi sanjari na kuwasaidia wazazi kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara.