2014-10-22 10:28:46

Mtakatifu Yohane Paulo II, Utuombee!


Tarehe 22 Oktoba 2014 kadiri ya Kalenda ya Liturujia, Kanisa limeadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, iliyotangazwa wakati Mtumishi wa Mungu Papa Yohane Paulo II alipokuwa anatangazwa kuwa ni Mwenyeheri na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 27 Aprili 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliwatangaza Papa Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa ni watakatifu katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kukusanya umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka ndani na nje ya Italia.

Ubalozi wa Poland mjini Vatican, unaendesha maonesho ya picha na nyaraka mbali mbali tangu maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican hadi Papa Yohane Paulo II alipotangazwa kuwa Mtakatifu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Poland wanakumbushwa kwamba, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ulimwengu na kwa namna ya pekee Poland imeendelea kukabiliwa na changamoto mbali mbali.

Na habari zaidi zinaonesha kwamba, Hospitali ya Gemelli ambako Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kupata tiba, imeamua kumuenzi Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kukipatia jina Kikanisa cha Hospitali hii kwa heshima ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Huu ni ushuhuda makini kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II jinsi alivyoweza kupokea mateso na mahangaiko yake kwa imani na matumaini, huku akiyaunganisha mateso haya na yale ya Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.