2014-10-22 14:22:44

Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 22 Oktoba 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ametafakari kuhusu mafundisho ya Mtakatifu Paulo kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo. Mwili wa binadamu ni mmoja, lakini umegawanyika katika viungo mbali mbali, hivi ndivyo ilivyo hata kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anasema, maono ya Nabii Ezekieli kuhusu mifupa mikavu kama inavyosimuliwa na Maandiko Matakatifu (Rej. Ez. 37:1-14) ambako Roho wa Bwana anaumba na kutoa uzima mpya kwa mifupa, ni kielelezo cha Kanisa ambalo limejazwa na karama ya maisha mapya kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa kushikamanisha na kuunganishwa kwa pamoja katika kifungo cha upendo.

Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanawezeshwa kuwa wamoja katika Fumbo la Mateso na Ufufuko wa Kristo; wanamshiriki Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, ambalo Kristo mwenyewe ndiye kichwa chake. Mtakatifu Paulo anatumia lugha ya picha kuonesha ukuu wa Fumbo hili kama unavyojidhihirisha upendo kwa wanandoa: pale ambapo Bwana na Bibi wanakuwa ni mwili mmoja, hivi ndivyo hali ilivyo kwa Kristo na Kanisa lake.

Kama viungo vya mwili mmoja, waamini wanaalikwa kuishi katika umoja, kwa kushinda kishawishi cha kinzani na utengano. Kwa kusukumwa na Roho Mtakatifu, Wakristo wajitahidi kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa katika fadhila ya upendo na kupokea kwa moyo wa shukrani zawadi nyingi kwa kuthamini zawadi zinazojionesha kutoka kwa waamini wengine pamoja na kuendelea kuonesha ukarimu kwa wale wote walioko kwenye shida na mahangaiko makubwa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili kweli waweze kuishi kikamilifu kama sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kusaidiana na kutaabikiana kwa pamoja kwa njia ya huduma makini.

Baba Mtakatifu akizungumza na mahujaji na wageni kutoka Poland amewakumbusha kwamba, tarehe 22 Oktoba 2014, kwa mara ya kwanza Kanisa limeadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, changamoto na mwaliko kwa wananchi wa Poland kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, ili kuipyaisha upya Poland na walimwengu waendelee kukimbilia huruma ya Mungu. Utajiri wake wa maisha ya kiroho uwahamasishe waamini kutafakari kuhusu mafao ya Kanisa, familia na Jamii kwa ujumla.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujitaabisha kuifahamu Injili, ili iweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya mtu binafsi na Jamii inayomzunguka pamoja na kutoa huduma makini kwa jirani. Ametambua uwepo wa wanafanyakazi kutoka Kampuni ya Ndege ya "Meridiana" wanaokabiliwa na matatizo na kinzani nyingi kwa wakati huu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, wafanyakazi hawa wataweza kupata suluhu ya kudumu kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kwa siku za usoni kwa kukazia utu na heshima ya binadamu pamoja na mahitaji ya familia nyingi.







All the contents on this site are copyrighted ©.