2014-10-21 15:13:49

Wakristo wanayo fadhila ya kumngoja Yesu kwa matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne tarehe 21 Oktoba, 2014, Siku kuu ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mwanzilishi wa Shirika la Wamissionari wa damu Azizi ya Yesu amesema kwamba, Wakristo ni watu wanaofahamu kumsubiri Yesu kwa imani na matumaini, kwani wanatambua kwamba, kwa njia ya sadaka yake Msalabani, amewakirimia uwezo wa kufanyika kuwa rafiki, jirani na wajenzi wa amani.

Tabia ya kungoja anasema Baba Mtakatifu inamjengea mwamini fadhila ya matumaini pamoja na kushikamana na Yesu kwa njia ya fadhila ya matumaini. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kuendelea kuimarisha urafiki, ili atakaporejea wakati wowote waweze kuwa tayari kumpokea na hatimaye kushiriki kikamilifu katika "mnuso" wa arusi wake, huku wakiwa na taa ambazo zinawaka. Yesu ameamua kujifanya kuwa mtumishi kwa kuhakikisha kwamba, anawahudumia waalikwa wote. Huduma ndio utambulisho ambao Yesu anapenda kuwakirimia wafuasi wake kama chapa ya kudumu katika hija ya maisha yao ya kiroho hapa duniani.

Kwa kushikamana na Kristo, waamini wanakuwa kweli ni marafiki wa Yesu wakiwa na majina na utambulisho kamili, kwani wote hawa wamekombolewa kwa njia ya Damu yake Azizi na hivyo kubomoa kuta za utengano ambazo zilikuwepo kati ya watu, ili wote waweze kuwa ni Familia ya Mungu, changamoto ya kuendelea kumngoja kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.