Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amefanya mikutano na wawekezaji kadhaa ambao
wanahudhuria mkutano wa uwekezaji barani Afrika ulioanza Jumatatu tarehe 20 Oktoba
2014 kwenye jijini London, Uingereza. Katika mikutano hiyo, Waziri Mkuu alikutana
na Mwenyekiti wa Taasisi ya Africa Matters Limited, Baroness Linda Chalker na kujadiliana
naye masuala yanayohusu utawala bora. Pia alikutana wawakilishi wa kampuni ya
Price Waterhouse Coopers (PwC) wakiongozwa na Bw. David Tarimo kutoka Tanzania, Bw.
John Gibbs (Kanda ya Afrika) na Bi. Anne Eriksson (Kanda ya Afrika Mashariki) na kuzungumza
nao masuala ya nishati na gesi asilia, miundombinu na upatikanaji wa rasilmali fedha
(mobilisation of resources). Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alikutana na mwanzilishi
na mweneyekiti wa kampuni ya Invest Africa, Bw. Robert Hersov pamoja na wenzake wanne
na kumweleza Waziri Mkuu nia yao kuwekeza Tanzania kwenye maeneo ya usindikaji mazao,
ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao na ufadhili wa miradi inayokubalika kiuchumi
na ambayo ni rahisi kupatiwa mikopo (Bankable projects). Naye Mtendaji Mkuu wa
kampuni ya Globeleq, Bw. Mikael Karlsson ambapo alimweleza Waziri Mkuu haja ya kampuni
hiyo kuzalisha umeme wa upepo kama njia mbadala ya kuongeza nishati hiyo badala ya
kutegemea gesi. Akijibu hoja zao kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe
wa timu hizo kwamba Tanzania ni mahali pazuri kwa uwekezaji lakini pia ni lazima pande
zote mbili ziwe makini ili kuhakikisha katika kila mradi inapatikana mizania sawia
ya maendeleo (win-win situation). Akizungumza na Bw. Karlsson wa kampuni ya Globeleq
Jumatatu, Oktoba 20, 2014, Waziri Mkuu alisema fursa ya kuzalisha umeme wa upepo iko
katika mikoa ya Singida, eneo la Makambako (Njombe), Katavi na Rukwa. “Sasa hivi
mbali ya upepo, mnaweza pia kuangalia uzalishaji wa nishati inayotokana na jotoardhi
(geo-thermal) katika eneo lililopo kwenye Bonde la Ufa. Kati ya megawati 40,000 zinazotarajia
kuzalishwa ndani ya eneo hili, megawati 5,000 ziko kwenye Bonde la Ufa la Tanzania”,
alifafanua. Kampuni ya Globelec pia inamiliki pia mitambo ya SONGAS ambayo inazalisha
umeme kwa kutumia gesi asilia. Waziri Mkuu aliwasili jijini London kuhudhuria mkutano
wa wakuu wa nchi unaohusu uwekezaji barani Afrika (The Global African Investment Summit
– TGAIS) kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete na ameshiriki mjadala huo pamoja na Rais
John D. Mahama wa Ghana, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Waziri Mkuu amefuatana na Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa Nishati
na Madini, Bw. Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba na Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu.