2014-10-21 09:39:31

Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya wanyonge huko Mashariki ya Kati!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 20 Oktoba 2014 katika kikao maalum cha Baba Mtakatifu na Makardinali kilichokuwa kinajadili kuhusu hali ilivyo huko Mashariki ya Kati amesema kwamba, hali kama ilivyo kwa sasa ni jambo ambalo haliwezi kamwe kukubalika na kwamba, wanao wajibu wa kimaadili kukemea kuhusu mateso, madhulumu na nyanyaso wanazofanyiwa watu huko Mashariki ya Kati. Watu wananyimwa haki zao msingi na kwamba, zawadi ya maisha, uhuru wa kidini, amani na utulivu vimetoweka huko Mashariki ya Kati.

Hali ya kisiasa huko Mashariki ya Kati ni tete kiasi cha kuhatarisha mfungamano wa Jumuiya ya Kimataifa. Mchakato wa amani huko Mashariki ya Kati hauna budi kuwa ni matunda ya upatanisho wa kitaifa, unaowajumuisha wadau mbali mbali, ili watu waweze kujifunza kuishi kwa amani, utulivu na mshikamano. Machafuko ya hali ya kisiasa huko Mashariki ya Kati hayawezi kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya mtutu wa bunduki, kwani kuna makampuni makubwa yanayoendelea kujinufaisha yenyewe kwa kufanya biashara haramu ya silaha katika maeneo ya vita. Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kimaadili wa kukomesha biashara ya silaha huko Mashariki ya Kati inayoendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kardinali Parolin anasema kwamba kuna makundi makubwa ya Wakristo yanayokimbia nchi zao huko Mashariki ya Kati kwa ajili ya kutafuta usalama wa maisha yao, jambo ambalo wakati mwingine linawatumbukiza katika mikono ya wafanyabiashara haramu ya binadamu. Inasikitisha kuona Mashariki ya Kati ikiwa haina tena Wakristo ambao wamekuwepo hapo kwa takribani miaka elfu mbili huku wakiungama imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Wakristo wamekuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa misingi ya amani, upatanisho na maendeleo. Ili Wakristo waweze kuendelea kuishi huko Mashariki ya Kati, kuna haja ya kuwajengea uwezo wa kuishi katika mazingira salama, wakiwa na fursa za ajira pamoja na kuwa na mikakati makini ya maendeleo kwa siku za usoni.

Kanisa kwa upande wake litaendelea kuonesha mshikamano wa upendo kwa njia ya sala, kwa kuhamasisha majadiliano na upatanisho, ili kweli amani na utulivu viweze kupatikana tena huko Mashariki ya Kati. Maelfu ya watu yanahitaji msaada wa hali na mali katika sekta ya elimu, afya na maendeleo, Kanisa hapa linapaswa kuonesha umoja na ushuhuda wa mapendo. Makanisa mahalia yaendelee kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga misingi ya haki, amani na utulivu.

Kardinali Parolin anasema kwamba Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kukaa kimya na kulifumbia macho matatizo na changamoto zinazojitokeza huko Mashariki ya Kati. Jumuiya hii inayowajibu wa kimaadili kusitisha vita na watu kuanza kujikita katika majadiliano yanayohimiza utekelezaji wa haki msingi kwa raia wote, kutafuta mafao ya wengi, kuheshimiana pamoja na kuthamini mchango unaotolewa na raia wote. Umoja wa Mataifa uhakikishe kwamba, hakuna mauaji ya kimbari yanayoweza kutokea huko Mashariki ya Kati pamoja na kuwasaidia Wakimbizi. Jumuiya ya Kimataifa ioneshe mshikamano wa dhati pamoja na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka kwa wote.

Mwishoni, Kardinali Pietro Parolin anasema kwamba, Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya matumaini kwa wale wote waliovunjika moyo kwa kushikamana nao katika sala pamoja na kuendelea kuwahimiza kubaki huko Mashariki ya Kati, kwa kutambua kwamba, wanao mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha mafao, maendeleo na ustawi wa wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.