Kanisa linahitaji rasilimali watu, vitu na fedha katika kazi ya Uinjilishaji!
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
wa watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari katika mahojiano maalum na
Radio Vatican wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani, iliyoadhimishwa
Jumapili iliyopita, tarehe 19 Oktoba 2014 anasema kwamba, Kanisa linahitaji rasilimali
watu, vitu na fedha kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa
mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Ni jukumu
la waamini katika Makanisa mahalia kuanza kujiwekea mikakati ya kulitegemeza Kanisa,
ili liweze kutekeleza vyema utume wake kati ya watu. Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari
yalianzishwa na Mama Kanisa, ili kuwahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika
kuchangia rasilimali watu, fedha na vitu katika kuendeleza kazi ya Uinjilishaji hadi
miisho ya dunia, sanjari na kuonesha mshikamano wa hali na mali na Makanisa mahalia.
Askofu
mkuu Rugambwa anasema kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa kuchangia
katika mfuko wa jumla wa shughuli za Uinjilishaji, ili kuyawezesha Makanisa machanga
kuendeleza dhamana na utume wa kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Wokovu, wakidhihirisha
matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Huu ni wajibu wa kila mwamini,
lakini pia waamini wanapaswa kuhamasishwa na kuelimishwa kuhusu ushiriki wao katika
kuchangia utume wa Uinjilishaji.
Askofu mkuu Protase Rugambwa anasema sadaka
na majitoleo haya ni muhimu sana katika kulitegemeza Kanisa mahalia sanjari na kushiriki
katika kuendeleza kazi ya Uinjilishaji inayohitaji rasilimali watu, vitu na fedha.