2014-10-20 12:14:50

Jengeni utamaduni wa mshikamano unaojikita katika misingi ya haki na amani!


Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini limewaandikia ujumbe waamini wa dini ya Kihindu kwa ajili ya Siku kuu ya Mwanga kama inavyojulikana "Deepavali" inayoadhimishwa tarehe 23 Oktoba 2014, ili mwanga kutoka juu, uweze kuwaangazia wao na majirani zao, ili kujenga na kudumisha utulivu, furaha, amani na maendeleo, kwa kujikita kwa pamoja katika utamaduni unaowakumbatia wote bila ya ubaguzi. Tema ya ushirikishwaji ni muhimu sana kwa watu wa nyakati hizi ambao wanakumbana na mifumo mbali mbali ya ubaguzi na kinzani.

Ni ukweli kwamba, utandawazi umefungua mipaka na kutoa fursa za maendeleo makubwa katika sekta ya elimu na afya. Umesaidia kukuza na kudumisha uelewa mkubwa wa demokrasia na haki jamii katika ulimwengu huu ambao kwa sasa unaonekana kama ulimwengu kijiji kutokana na maboresho ya njia za mawasiliano na usafiri. Kwa hakika mchakato wa utandawazi haujafanikiwa kufikia lengo la kuwajumuisha watu mahalia katika Jumuiya ya Kiulimwengu na matokeo, imechangia kuwafanya watu wengi kupoteza utambulisho wao wa kijamii na kitamaduni; kiuchumi na kisiasa.

Utandawazi umekuwa na athari kubwa hata katika Jumuiya za kidini kwani hata hizi pia ziko duniani. Jamii nyingi zimemeguka na hivyo kusababisha ubinafsi na mawazo mepesi mepesi kutawala, kiasi cha kuifanya dini kuwa ni jambo binafsi lisilokuwa na mvuto wala mguso kwa Jamii husika. Kumekuwepo na ongezeko la misimamo mikali ya kidini na kiimani pamoja na ukabila, mambo yanayokatisha tamaa; ongezeko la wasi wasi kuhusu usalama miongoni mwa Jamii, lakini zaidi kati ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kundi ambalo bado halijafaidika na fursa za utandawazi.

Utandawazi umechochea ulaji wa kupindukia na tabia ya watu kupenda mali na hivyo kumezwa na malimwengu. Ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; ukosefu wa haki msingi pamoja na baadhi ya watu ndani ya Jamii kusababisha mateso kwa jirani zao. Huu ndio utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Ulimwengu mamboleo unasheheni kundi kubwa la maskini ambao wananyimwa haki zao msingi; fursa na rasilimali ambayo inapatikana kwa wanajamii wengine. Kundi hili linaonekana kuwa ni mzigo wa Kijamii, kundi lisilopendwa wala kuthaminiwa.

Katika mfumo kama huu wa maisha, kuna watoto na wanawake wanaonyanyaswa; wazee wasiotunzwa wala kuheshimiwa, wagonjwa, walemavu, wahamiaji na wakimbizi; kuna makundi ya waamini yanayoendelea kudhulumiwa kutokana na imani yao; mambo yote haya ni kielelezo cha kukua na kukomaa kwa utamaduni wa ubaguzi.

Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini linasema, mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa mshikamano ni mwaliko kwa wote, unaojikita katika uwajibikaji wa pamoja unaopaswa kufanyiwa kazi. Huu ni mradi unaopania kutunza afya na ustawi wa Familia ya binadamu licha ya nguvu ya utamaduni wa ubaguzi inayoendelea kutikisa maisha ya mwanadamu kwa nyakati hizi. Wakristo na Wahindu kwa kushirikiana na waamini wa dini mbali mbali wanaweza kujenga utamaduni wa mshikamano ili kujenga jamii inayosimikwa katika msingi wa haki na amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.