2014-10-20 10:54:34

Hati ya Mababa wa Sinodi maalum kuhusu Familia imechapishwa!


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kuchapishwa kwa Hati ya Mababa wa Sinodi ambayo ni mkusanyiko wa mawazo ya wajumbe binafsi na yale yaliyokusanywa katika majadiliano ya vikundi; hati ambayo kwa lugha ya kitaalam inajulikana kama "Relatio Synodi".

Hiki ni kielelezo cha ukweli na uwazi, ili kuonesha ni wapi ambapo Mababa wa Sinodi wamekubaliana kimsingi na pale ambapo wameonesha kugawanyika kutokana na mitazamo na tamaduni za watu. Mababa wa Sinodi waliweza kufanya marekebisho 470 yaliyowasilishwa kwenye vikundi vidogo vidogo kutoka kwenye Hati Elekezi iliyotolewa mara tu baada ya maadhimisho ya Sinodi katika Juma la kwanza la kazi.

Hati ya Mababa wa Sinodi sehemu ya kwanza inaonesha: Umuhimu wa Kanisa kusikiliza: mintarafu mazingira na changamoto za maisha ya kifamilia: Hapa Mababa wa Sinodi wanaangalia mazingira ya kijamii na kitamaduni; umuhimu wa hisia katika maisha ya watu pamoja na changamoto za kichungaji zinazoendelea kujitokeza ndani ya Kanisa.

Sehemu ya Pili ya hati hii, inamwangalia Kristo, ili kuliwezesha Kanisa kutangaza Injili ya Familia. Hapa Mababa wa Sinodi wanaelezea mpango wa Mungu katika historia ya ukombozi; familia kama kielelezo makini cha mpango wa ukombozi. Mababa wanaangalia familia kama ilivyojadiliwa katika Nyaraka mbali mbali za Kanisa.

Wanatambua kwamba, kiini cha Sakramenti ya ndoa ni upendo usiogawanyika na kwamba, ndoa ni zawadi ya kudumu ambayo inawaalika wanandoa kuifurahia kwa kuishi kwa pamoja. Wanandoa wanapaswa kutambua kweli na uzuri wa maisha ya ndoa na familia kwa kuendelea kujikita katika huruma ya Mungu ili kuponya madonda na mapungufu yanayojitokeza katika maisha ya binadamu.

Sehemu ya tatu ya Hati ya Mababa wa Sinodi inapembua kwa kina na mapana mikakati ya kichungaji, ili kuliwezesha Kanisa kutangaza Injili ya Familia katika ulimwengu mamboleo na kati ya watu wanaoishi katika mazingira tofauti. Mababa wa Sinodi wanaliomba Kanisa kuwasindikiza kwa moyo wa unyenyekevu wanandoa watarajiwa katika mchakato wa maandalizi ya ndoa; kuendelea pia kuwasindikiza katika maisha haya katika miaka yao ya kwanza kwanza ya maisha ya ndoa na familia.

Kanisa halina budi kubainisha mikakati ya kichungaji kwa ajili ya wale waliofunga ndoa Serikalini na wale ambao bado wanaishi "uchumba sugu". Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa lisaidie kutibu madonda ya wanandoa waliotengana na kuamua kuoa au kuolewa tena; familia tenge, yaani zinazosimamiwa na mzazi wa upande mmoja.

Kanisa lioneshe jicho la huruma kwa watu wenye mielekeo ya kuwa na mahusiano ya jinsia moja. Mama Kanisa anapenda kukazia umuhimu wa familia kurithisha zawadi ya maisha na changamoto zilizopo katika kupanga uzazi. Mwishoni, Mababa wa Sinodi wanaangalia changamoto ya elimu na dhamana ya Familia katika Uinjilishaji.

Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anasema kwamba, vipengele vyote sitini na viwili, vilipigiwa kura na Mababa wa Sinodi 183. Kati ya vipengele hivi, pendekezo la wanandoa waliotalakiana na hatimaye kuamua kuoa au kuolewa kushiriki katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, halikuungwa mkono na Mababa wengi wa Sinodi na limeamriwa kwamba, litajadiliwa kwa kina wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya kawaida ya Maaskofu, hapo Oktoba, 2015. Mababa wa Sinodi wamekataa kufananisha ndoa za watu wa jinsia moja na Sakramenti ya ndoa.







All the contents on this site are copyrighted ©.