2014-10-19 08:03:03

Serikali ya Vietnam inalipongeza Kanisa kwa kushiriki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Vietnam


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi mchana alikutana na kuzungumza na Bwana Nguyen Tan Dung, Waziri mkuu wa Vietnam ambaye baadaye pia alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu na mgeni wake wamepongeza hatua ambayo imefikiwa kati ya nchi hizi mbili katika mchakato wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili tangu Waziri mkuu wa Vietnam alipotembelea kwa mara ya kwanza Vatican kunako mwaka 2007. Vietnam inalishukuru Kanisa kwa mchango wake katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Vietnam katika ujumla wao. Kanisa linaishukuru Serikali kwa ushirikiano uliopo mintarafu Katiba ya nchi ya Mwaka 2013 katika masuala ya kidini.

Mwakilishi wa Vatican nchini Vietnam asiye mkazi ameendelea kuchangia kwa karibu zaidi katika kukuza mahusiano mema kati ya Serikali na Kanisa, wakilenga zaidi katika kuimaarisha ushirikiano wa kidiplomasia. Viongozi hawa wawili kwa pamoja wamejadili masuala msingi yatakayofanyiwa kazi na pande hizi mbili katika siku za usoni kwa kuendelea kutumia njia za mawasiliano zilizopo hadi wakati huu.

Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamebadilishana mawazo kuhusiana na masuala mbali mbali yanayoendelea kutikisa Kikanda na Kimataifa, lakini kwa namna ya pekee wameangalia sera na mikakati inayochukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kujenga na kudumisha misingi ya amani na utulivu Barani Asia.







All the contents on this site are copyrighted ©.