Mwenyeheri Papa Paulo VI alikuwa ni Nabii shupavu!
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Mwenyeheri Papa Paulo VI alikuwa
ni Nabii shupavu aliyekuwa na mwono mpana katika kulinda, kutetea na kuendeleza utu,
heshima na zawadi ya uhai wa binadamu kadiri ya mpango wa Mungu.
Mwenyeheri
Paulo VI katika maisha na utume wake, alikazia umuhimu wa binadamu kuzingatia mpango
wa Mungu katika kazi ya uumbaji kwa kujikita katika mpango wa uzazi kwa njia ya asili
ili kupunguza "majanga" mbali mbali yanayoweza kusababishwa na tabia ya kukumbatia
utamaduni wa kifo kwa kuenzi sera za utoaji mimba. Alitetea maisha ya ndoa na familia,
akawataka wanandoa kudumisha upendo wa dhati kwa kuenzi uhai.
Hili ni jukumu
la waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda,
kutetea na kudumisha zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti
ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Ni wajibu wa watu wenye mapenzi
mema kukataa katu katu misaada inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; misaada
inayokwenda kinyume cha kanuni maadili.