2014-10-18 09:25:08

Wasifu wa Mtumishi wa Mungu, Paulo VI


Giovanni Battista Montini, alizaliwa kunako tarehe 26 Septemba 1897 huko Concesio, Brescia, Kaskazini mwa Italia. Baada ya mafunzo na majiundo yake ya kikasisi akapadrishwa kunako tarehe 29 Mei 1920. Baada ya kujiendeleza katika masomo ya Falsafa mjini Roma na Sheria mjini Milano, kunako mwaka 1923 hadi 1924 alianza utume wake kwenye Sekretarieti ya Vatican na kutumwa kwenda kufanya kazi kwenye Ubalozi wa Vatican mjini Varsavia, Poland.

Montini alikuwa ni mshauri wa Shirikisho la Vyama vya Wanafunzi Wakatoliki Italia, utume alioutekeleza kati ya mwaka 1925 hadi mwaka 1933. Katika kipindi cha mwaka 1920 hadi mwaka 1930 alibahatika kufanya hija nyingi za maisha ya kiroho na kitamaduni ndani na nje ya Italia.

Katika utekelezaji wa majukumu yake ndani ya Sekretarieti ya Vatican, Giovanni Montini alibahatika kupendwa na kuthaminiwa na Papa Pio kumi na moja pamoja na Papa Pio wa kumi na mbili. Tarehe 13 Desemba 1937 akateuliwa kuwa ni Katibu mkuu msaidizi wa Vatican; na kati ya Mwaka 1930 hadi mwaka 1937 alifundisha historia ya diplomasia ya Kanisa kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Laterano, kilichoko mjini Roma.

Katika kipindi cha miaka kumi ya kazi za kidiplomasia, alijibidisha sana kukuza na kuimarisha utume wake wa Kipadre na kama kiongozi wa maisha ya kiroho; akawa ni mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa matendo ya huruma na mshiriki mkuu wa Chama cha Mtakatifu Vincent wa Paulo. Wakati wa vita kuu ya Pili ya Dunia alitoa msaada mkubwa kwa Wayahudi na mara tu baada ya vita, akawa ni muasisi wa Chama cha Wafanyakazi Wakatoliki Italia, akahamasisha uanzishwaji wa vyama vya kisiasa vyenye mwelekeo wa kukuza na kuimarisha mafundisho ya Kanisa Katoliki pamoja na kuanzisha mchakato wa chama cha walei kimataifa.

Tarehe 29 Novemba 1952 aliteuliwa kuwa ni Katibu wa mambo ya kawaida mjini Vatican na tarehe Mosi, Novemba 1954 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano na kuwekwa wakfu tarehe 12 Desemba 1954. Katika maisha na utume wake, akajikita zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji, huduma kwa wahamiaji, akajenga Makanisa na kuimarisha waamini.

Alibahatika kufanya hija mbali mbali: Marekani, Brazil na Afrika. Tarehe 15 Desemba 1958 akateuliwa kuwa ni Kardinali na Papa Yohane wa XXIII, akapewa dhamana ya kuanzaa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ambayo yalikuwa ni mwanzo wa mageuzi makubwa ndani ya Kanisa.

Tarehe 21 Juni 1963 akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na kuchagua jina la Paulo VI, akashiriki kukamilisha awamu tatu za Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, licha ya matatizo na changamoto nyingi kwa wakati huo, akaonesha ujasiri mkubwa kwa kufungua malango ya Kanisa kwa ajili ya ulimwengu mamboleo, huku akikazia umoja na mshikamano ndani ya Kanisa. Alibahatika kufanya hija za kichungaji, akianzia Nchi Takatifu alikokutana na Patriaki Anathegoras wa Yerusalem, huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa.

Aliwahi kutembelea India, Makao makuu ya Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1965, Fatima na Uturuki mwaka 1967; Colombia mwaka 1968, Geneva na Uganda mwaka 1969. Aliwahi pia kutembelea Mashariki ya Mbali, Australia na Oceania kunako mwaka 1970. Alitembelea majimbo mengi ya Italia, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo.

Papa Paulo VI aliandika Waraka wake wa kwanza "Ecclesiam Suam" Kanisa la Kristo kunako mwaka 1964, akafungua mbinu ya majadiliano ya wokovu ndani ya Kanisa na Walimwengu. "Mysterium Fidei" ni Waraka juu ya umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ulioandikwa kunako mwaka 1965; "Mense Maio" Mwezi Mei, Ibada kwa Bikira Maria, Waraka wa Mwaka 1965 na kunako mwaka 1966 aliandika Waraka wa "Christi Matri, kwa ajili ya Bikira Maria ili aweze kuombea amani duniani.

Waraka wa "Populorum progressio" kwa ajili ya Maendeleo ya Watu, uliochapishwa kunako mwaka 1967 na "Humanae Vitae" wa mwaka 1968 uliojikita katika ndoa na mpango wa uzazi. Alijitahidi kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kuanzisha Siku ya Kuombea Amani Duniani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari.

Papa Paulo VI aliteseka kwa shida na changamoto zilizolikumba Kanisa wakati wa uongozi wake, akaonesha ari na moyo wa ujasiri kushuhudia imani katika matendo, akionesha uthabiti wa Mafundisho ya Kanisa katika kukabiliana na changamoto za mifumo na sera mbali mbali duniani. Alitangaza Mwaka wa Imani, ulioadhimishwa kuanzia mwaka 1967 hadi mwaka 1968 na kuchapisha Kanuni ya Imani ya Watu wa Mungu kunako mwaka 1968. Alionesha uwezo mkubwa katika kusuluhisha masuala mbali mbali, unyenyekevu katika kufanya maamuzi pamoja na kukazia kanuni msingi, akawa tayari kuwapokea wale walioelemewa na ubinadamu wao.

Ni kiongozi aliyeguswa na mahangaiko ya wafanyakazi, akaonesha mchango mkubwa wa Kanisa katika kukabiliana na masuala mbali mbali ya kijamii na kiuchumi, akachapisha Waraka wa Mikakati ya Uinjilishaji, ujulikanao kama "Evangelii nuntiandi" unaogusa mateso na mahangaiko ya maskini. Alisimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; akakemea talaka na utoaji mimba. Alipambana na kinzani zilizojitokeza katika baadhi ya mataifa sanjari na kukema vitendo vya kigaidi.

Papa Paulo VI alikuwa ni mnyenyekevu, mtu wa watu na mchamungu; alijenga maisha yake ya kiroho katika: Maandiko Matakatifu, Mababa wa Kanisa na Watakatifu; akashuhudia imani thabiti, matumaini na mapendo. Sala yake ilijikita katika Neno la Mungu, Liturujia na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; alikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Kanisa, kiasi hata cha kuchapisha Waraka wa Ibada kwa Bikira Maria, "Marialis Cultus" kunako mwaka 1974. Mwanzoni mwa utume wake, aliwahimiza vijana wa kizazi kipya na waamini wote kwa ujumla kuchuchumilia furaha ya imani na kujichimbia katika utamaduni wa upendo.

Alifariki dunia kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo kunako tarehe 6 Agosti 1978 baada ya kuugua kwa muda mfupi. Alifariki dunia huku akiwa anasali Sala ya Baba Yetu na Wosia wake alitafakari kuhusu kifo, hazina kubwa katika maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akatambua karama zake za kishujaa hapo tarehe 20 Desemba 2012.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.