2014-10-18 07:18:00

Papa Paulo VI alikazia mchakato wa Uinjilishaji wa watu!


Askofu mkuu Protase Rugambwa Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Papa Paulo Vi ambaye anatangazwa na Mama Kanisa kuwa Mwenyeheri, alikazia sana umuhimu wa kukuza na kuimashirika miito mitakatifu ndani ya Kanisa pamoja na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu baina ya Makanisa kama kikolezo cha utekelezaji mikakati ya Uinjilishaji duniani. RealAudioMP3

Papa Paulo VI alikazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa Kanisa kuwaandaa barabara waamini walei kwa kuwajengea ari na moyo wa kimissionari, tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kushiriki katika azma ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa kuwashirikisha wengine ile Injili ya Furaha kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko. Waamini walei wanaendelea kuhamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama chachu ya kuyatakatifuza malimwengu.

Askofu mkuu Rugambwa anasema, kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha ni kivutio kikubwa na changamoto endelevu ya kumwilisha Mafundisho ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu. Papa Paulo VI alikazia umuhimu wa mchakato wa maendeleo ya watu: kiroho na kimwili; Injili ya uhai; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu dhidi ya utamaduni wa kifo.

Askofu mkuu Rugambwa, anaendelea kusema kwamba, amani na maendeleo ni mambo ambayo yamekuwa yakipewa mkazo wa pekee na viongozi mbali mbali wa Kanisa. Amani, ikimwilishwa kikamilifu katika vipaumbele vya maisha ya watu ni kikolezo kikuu cha maendeleo ya watu.

Hii ndiyo pia changamoto ambayo nchi nyingi za Kiafrika inakabiliana nayo na kwa namna ya pekee Tanzania wakati huu inapoendelea na mchakato wa kuandika Katiba mpya, itakayokuwa ni sheria mama. Katiba mpya ichangie kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano, utu na heshima ya binadamu, daima mafao na ustawi wa wengi vikipewa msukumo wa pekee.







All the contents on this site are copyrighted ©.