2014-10-18 12:17:47

Dunia ina kiu ya kusikiliza Injili inayoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha!


Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Italia, kwa kifupi "FUCI" katika maadhimisho ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Paulo VI kuwa Mwenyeheri, liliandaa kongamano la kitaifa kwa ajili ya kumuenzi Mtumishi wa Mungu Paulo VI ambaye aliwahi kuwa Mshauri wake wa maisha ya kiroho kuanzia mwaka 1925 hadi mwaka 1933 huko Arezzo, Italia. Kongamano hili limeongozwa na kauli mbiu "Roho na Ukweli" kama sehemu ya changamoto endelevu kwa wasomi katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya amewatumia wanafunzi hawa ujumbe maalum akiwataka kujikita katika mambo makuu matatu: Masomo, Tafiti na Utume, mambo msingi katika maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu, wanaojibidisha kusoma kwa juhudi, bidii na maarifa; mambo muhimu sana yanayomwezesha mwanadamu kufikia ukweli, wema na uzuri.

Vijana wasomi wa kizazi kipya wasiridhike kuyapata mambo haya nusu nusu, bali wajibidishe kuyatafuta katika undani wake wote. Ili kufanikisha juhudi hizi kuna haja kwa wanafunzi kuonesha unyenyekevu unaojikita katika kusikiliza kwa makini. Masomo yawasaidie wanafunzi kutambua kweli za maisha ili waweze kuwajibika zaidi. Hapa Baba Mtakatifu anawataka vijana kusoma kwa bidii, juhudi na maarifa, huku wakiwa na matumaini.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana wasomi kwamba, wanapaswa kufanya tafiti zinazojikita katika majadiliano ya kina pamoja na upembuzi yakinifu. Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Italia limeonesha ari na moyo wa unyenyekevu katika tafiti zao; wakiwa wazi kutembea kwa pamoja na wale wote wanaotafuta ukweli katika mwanga wa imani. Tafiti makini zinawawezesha wahusika kukutana na mwanga wa imani, akili na sayansi katika mjadala wenye kujenga uwiano mzuri kati yake. Tafiti za kisayansi zinafanywa katika dhamiri nyofu na wazi, ili kugundua utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Injili na tamaduni mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wasomi kwamba, tamaduni za ulimwengu mamboleo zina kiu sana ya kusikiliza Habari Njema ya Wokovu; inayoangazwa kwa shuhuda makini, ili kujenga na kuimarisha utu wa mtu.

Baba Mtakatifu anasema Chuo kikuu ni mahali ambapo kunawafungulia wasomi milango ya utume na shughuli mbali mbali kwa ajili ya siku za usoni, changamoto ya kujitaabisha kwenda hadi pembezoni mwa Jamii ili kuponya madonda ya umaskini yanayojikita katika mambo msingi ya binadamu. Wasoni wajitaabishe kujenga utamaduni wa kukutana na kukaribisha, kwa kushirikishana furaha na matumaini; mateso na mahangaiko ya ndani.

Hakuna haja ya kuweka vikwazo au vizingiti katika mipaka hii, bali kufungua mlango wa matumaini ya kazi, ushirikiano na majadiliano. Ulimwengu mamboleo unahitaji watu kushikamana na kutembea kwa pamoja, ili kuondokana na falsafa za kinzani na migongano isiyokuwa na tija wala mashiko katika ustawi na maendeleo ya binadamu.

Ni changamoto na mwaliko wa kujenga na kuendeleza utamaduni wa kukutana pamoja na udugu, ili kuwamegea wengine Injili na utamaduni kuweza kuufikisha katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka wasomi kuwa na matumaini kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi, kwa kushiriki kikamilifu katika kuleta mageuzi ndani ya Jamii na Kanisa katika ujumla wake. Hapa kunahitajika moyo na ari ya ujasiri, unyenyekevu na kusikilizana kama vielelezo makini vinavyopania kuleta mabadiliko katika Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.