Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea Sh. Bilioni 10.1 ambazo ni sawa
na EURO milioni 4.8 kutoka Serilkali ya Finland ikiwa kwa lengo la ushirikiano wa
Mpango wa Mageuzi ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM) Awamu ya IV.
Mkataba
wa makubaliano hayo umesainiwa Alhamisi tarehe 16 Oktoba 2014 Jijini Dar es salaam
na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Doroth Mwanyika kwa niaba ya Serikali ya
Tanzania na Balozi wa Finland nchini Bi. Sanikka Antila. Bi. Doroth amesema kuwa
Mpango wa Mageuzi ya Usimamizi wa Fedha za Umma Awamu ya nne ametanguliwa na Awamu
ya I hadi III ambapo awamu hizo zimeonesha mafanikio mbalimbali nchini Tanzania.
Mafanikio
hayo ni pamoja na ongezeko la ukusanyaji wa mapato kutoka Sh. Bilioni 390 mwaka 2009/2010
hadi zaidi ya Sh. Bilioni 700 kwa mwezi mwaka 2013/2014 na kuboresha mifumo ya kifedha
kwa kutumia mifumo ya kielektroniki kwa kulipa moja kwa moja kwenye akaunti husika.
Bi
Doroth metaja mafanikio mengine kuwa ni ubureshwaji wa utendaji watumishi wanaosimamia
masuala ya mpango wa PFM kupitia Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali
(CAG) na utendaji kazi mzuri wa kamati za Bunge zinazohusika na ufuatiliaji wa matumizi
ya Fedha za umma.
Aidha, Bi. Doroth ameishukuru Serikali ya Finland kwa ushirikiano
mzuri wanaoendelea kuipa Tanzania na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika katika malengo
yaliyokusudiwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kupunguza umasikini nchini.
Naye
Balozi wa Finland nchini Bi. Sanikka Antila amesema kuwa usimamizi mzuri wa fedha
za umma (PFM) umeifanya nchi yake kuongeza fedha kwa ajili ya mpango huo. “PFM ni
muhimu kwa utawala wa kidemokrasia, uchumi imara, ufanisi katika matumizi ya rasilimali
zilizopo na hivyo kupunguza umasikini” alisema Bi. Sanikka. Ufanisi wa usimamizi mzuri
wa fedha za umma umewezesha ufanisi wa malighafi zilizopo nchini katika kuboresha
elimu, kutoa huduma bora za kiafya, kuongeza mazao ya kilimo na kuendeleza utalii.
Mpango
wa PFM upo katika awamu ya nne na ulianza 2012 na unatarajiwa kuishia 2017 ambapo
awamu ya I hadi III ilianza 1998 na kumalizika 2012, Finland imekuwa nchi ya sita
mhisani katika kusaidia mpango huu wa mageuzi. Nchi nyingine wahisani ni pamoja na
Canada, Ujerumani Ireland na Uingereza.