2014-10-17 14:33:23

Kanisa litaendelea kusimama kidete kutangaza Injili ya uhai!


Kimaumbile upendo wa kindoa ni kwa ajili ya kukuza na kuendeleza Injili ya uhai, dhamana ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuitangaza na kuishuhudia kwa njia ya maisha adili na matakatifu, dhamana inayojidhihirisha kwa kuzaa na kulea watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Familia inayoundwa kutokana na ndoa ni kweli mahali pa utakatifu wa maisha, hapa ni mahali ambapo uhai ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu unapokelewa na kulindwa dhidi ya hatari na vikwazo vinavyoweza kujitokeza.

Familia ina wajibu na dhamana ya kujenga na kukuza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa hivi, Familia za Kikristo, kwa wema wa Sakramenti zinapokea wito wa pekee ambao unazifanya ziwe ni mashahidi wa kutangaza Injili ya Uhai, hasa wakati huu, dunia inapoendelea kumezwa na malimwengu kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Mwenyeheri Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II wawe ni mfano na kielelezo cha kuigwa katika kutangaza Injili ya Uhai, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha, utu na heshima ya binadamu.

Kwa kutambua wajibu na dhamana hii, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaowanyemelea wananchi wa Kenya kwa sasa. hayo yamebainishwa hivi karibuni na Askofu Salesius Mugambi, Mwenyekiti wa Tume ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya. Wananchi wanapaswa kutambua kwamba, wao ni sehemu ya kazi ya uumbaji na kwamba, wanawajibika kulinda na kutunza mazingira, lakini kwanza kabisa zawadi ya maisha, kwani binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu Mugambi ameyasema haya wakati akishiriki katika matembezi ya kuenzi zawadi ya maisha ambayo kwa mwaka huu yameongozwa na kauli mbiu "maisha ya binadamu ni matakatifu, tuyalinde".

Haki ya kuishi ni kati ya mambo yaliyobainishwa kwenye Katiba mpya ya wananchi wa Kenya; watoto ambao hawajazaliwa, utu wao unapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa. Askofu Mugambi ameonya pia tabia ya kuzuka kwa biashara haramu ya binadamu na kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuwa macho dhidi ya tabia hii inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Ameitaka Serikali kuangalia pia tatizo la watoto kufanyishwa kazi katika mazingira hatarishi na magumu, mambo yanayodumaza ustawi na maendeleo ya watoto hawa.

Askofu Mugambi amegusia pia matatizo kama nyanyaso za kijinsia, ulevi wa kupindukia, utamaduni wa kifo na ukosefu wa ajira kuwa ni kati ya matizo na changamoto zinazozikabili familia nyingi nchini Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.