Wakati wa Yesu kulikuwa na makundi ya watu yenye itikadi za kidini na kisiasa zinazopingana.
Kati ya makundi hayo kulikuwa Wafarisayo na Maherodi. Makundi haya mawili tungeweza
kuyalinganisha na vyama vya upinzani vyenye itikadi na sera tofauti za kisiasa katika
nchi.
Leo tutawaona viongozi wa vyama hivyo wakiungana pamoja ili kuihujumu
serikali. Watu wa vikundi hivyo vya Wafaisayo na Maherodi pamoja na mashabiki wao
wakamwendea Yesu mtu wa kweli na haki kama wanavyoanza kumrubuni kwa lugha nzuri wanamwambia:
“Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika
kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.” Baada
ya kumwagia sifa hizo ili ashabikie ufisadi wao wakamwuliza swali la kifisadi: “Basi
utuambie, waonaje ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?”
Katika Injili ya
Luka suala la kodi na ushuru lilikuwa nyeti sana, na ndilo walilomshtakia Yesu kwa
Pilato kusudi auawe: “Wakaanza kumshitaki, wakisema, ‘Tumemwona huyu akipotosha taifa
letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo
Mfalme.’” (Lk.23:2) Swali hili lilikuwa na mtego ulio mgumu sana kuuepa, kwani lilimbana
Yesu katika masuala mawili mazito na nyeti yanayoikabili kila nchi yaani katika uwanja
wa kiuchumi na wa kisiasa.
Ingawaje ulipaji kodi au ushuru ni suala la toka
zamani za mababu zetu lakini zoezi hili limebaki kuwa nyeti na linalokera sana wananchi
popote ulimwengu, hasa kutokana na jinsi linavyogusa uchumi binafsi. Kwa hiyo kutokana
na unyeti wake, suala hili linasababisha kuwa na migomo na maandamano ya mara kwa
mara katika nchi. Kuhusu kero hiyo ya ulipaji wa kodi tunaweza kuiona kidogo tukifuatilia
makala ya mwanahistoria myahudi Yosefu Flavio, aliyeishi kipindi walichokuwa wanaishi
mitume.
Mwanahistoria huyu anasimulia vituko mbalimbali ambavyo viliwahi kutokea
huko Palestina wakati wake, vituko vilivyoibua migomo na maandamano kadhaa kule Palestina
dhidi ya ulipaji kodi kwa serikali ya kikoloni. Ananukuu kituko kile cha Yuda wa Galla
kinachosimuliwa pia katika kitabu cha Matendo ya Mitume, kulipokuwa na sensa ya Kwirinus,
kwa ajili ya kujua idadi ya watu wa kulipa kodi.
Suala lenyewe la kuhesabu
watu halikukubalika kwa Wayahudi, hata Daudi anaomba radhi kwa kosa hilo, kwani ni
Mungu peke yake anayo mamlaka juu ya mtu kwa sababu hakuna mtu yeyote duniani mwenye
mamlaka juu ya mwingine. Ulipaji kodi uyahudini ulileta maudhi zaidi kwa vile uligusa
itikadi ya dini yao, kwani katika sarafu ya fedha kuliandikwa maneno yaliyo kinyume
na imani kwa Mungu mmoja. “….” Upande wa pili “Sommo Pontefice” na picha ya mwanamke
aliyekaa, alama ya amani, yawezekana mwanamke huyo alikuwa ni mama wa mwenyewe Tiberius.
Kwa wayahudi kuitumia sarafu hiyo ilikuwa kama kuabudu miungu ya uongo.
Katika
mazingira kama hayo, ndiyo linaingia swali la mafisadi hao ili wamwingize Yesu mkenge,
yaani wamgonganishe na utawala (kwa kutolipa kodi), na aingilie kuchafua utaratibu
wa uchumi. Huo ni ufisadi kwani unataka kumpa mtu mwanya wa kuepa wajibu wake wa kulipa
kodi kwa serikali. Aidha ni swali la kisiasa kwa vile linataka kumgombanisha Yesu
na Kaisari pamoja na taifa lake la wayahudi.
Kwa vyovyote Mafisadi hawa walijua
wazi kwamba wanawajibika kulipa kodi kwa serikali yao, lakini kwa bahati mbaya serikali
yao ilikuwa ya wakoloni wa kirumi. Walilazimika kulipa kodi chini ya utawala wa warumi
tena kwa kutumia pesa ya nuksi kwani ilikuwa na sura ya mfalme Tiberius aliyejidai
kuwa mungu.
Kwa vile ni swali la kihuni, Yesu naye anacheza na uhuni wao bila
wao kujitambua. Anaomba kuoneshwa sarafu ya pesa. Kwa kufanya hivyo yaonesha kwamba
yeye mwenyewe alikuwa fukara, hakuwa na pesa mfukoni. Lakini wao walikuwa nayo na
walikuwa wanaitumia ndiyo maana wanachomoa mifukoni mwao na kumpa. Mbaya zaidi walikuwa
katika mazingira ya hekaluni (kanisani) sehemu takatifu (Mt. 21:23).
Hawaogopi
kutia nuksi Kanisani kwa kuonesha pesa yenye picha ya mfalme Kaisari. Hapo wanaonesha
jinsi walivyo wanafiki kwa sababu wanakuwa na uangalifu tu wanapotakiwa kulipa kodi
na ushuru. Yesu baada ya kuichunguza pesa ile, anawauliza: “Ni ya nani sanamu hii?”
Wanapomjibu kuwa ni ya Kaisari, anawaambia: “Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari,
na Mungu yaliyo ya Mungu.” Jibu hili la Yesu linajulikana na watu wote hata wasio
wakristu, hasahasa wana siasa na watu wa serikali, na wanafasiri kadiri inavyowapendeza
wao.
Hao wanasema kuwa Yesu alimaanisha kuwa “dini isiingilie mambo ya serikali
na siasa” na watu wa dini wanasema kwamba Yesu alimaanisha kwamba dini inamwakilisha
Mungu na hivi inayo mamlaka hata upande wa siasa na dini.” Hebu tuone Yesu mwenyewe
alimaanisha nini.
Kuna ujumbe au mafundisho mawili yayopatikana katika jibu
hili: Mosi, ni dhahiri kabisa kwamba, kulipa kodi ni wajibu wa kimaadili licha ya
wajibu wa kiraia kuchangia kutokana na tunachotendewa na jamii hiyo. Hakuna hoja yoyote
ya haki au utetezi wowote ule wa kutolipa kodi au ushuru. Hata kama uongozi wa serikali
ungekuwa ovyo na wa kidhuluma.
Kumbe, kiuchumi na kisiasa, wanafunzi wa Kristo
wameitwa kuwa raia waaminifu na wenye kutoa mfano wa kuwajibika katika kujenga jamii
yenye haki na upendo. Mkristo daima achague siasa inayowapendelea zaidi wanyonge,
siyo ile inayohifadhi maslahi yake tu.
Ndiyo maana Paulo anawaandikia warumi-
katika kipindi ambacho Roma ilikuwa imeanza kutawaliwa na mfalme Nero – akiwa bado
kijana tu wa miaka 20 tu na kwa muda kidogo wa miaka mitatu ya utawala wake, anawahimiza
wakristu wa Roma akisema: “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka
isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamriwa na Mungu.
Hivyo amwasiye mwenye
mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu…Kwa hiyo
ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri. Kwa
sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika
kazi hiyo hiyo. Wapeni waote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye
hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima;” (War. 13:1-7).
Kwa jibu hilo Yesu
anataka kutuasa juu ya kuwajibika, yaani, kama umepewa huna budi kurudisha. Kama umepokea,
yabidi kurudisha. Ninyi mnatumia hela iliyo mali ya serikali ya kirumi. Serikali hiyo
inawatengenezea barabara, inawahakikishia usalama wa raia, yaani ina askari wanaowalinda,
inawaendeshea biashara, na mambo yanaenda sawa. Mmepokea haya yote sasa rudisheni,
maana yake lipeni kodi zote kutokana na huduma mnayopata hakuna hoja ya kuepa kulipa
kodi au ya kutokutoa ushuru.
Kwa hiyo siyo hakikuepa kutoa ushuru ba kulipa
kodi. Tunaweza pia kuwaasa mafarisayo wa leo wanaoepa kulipa kodi na kutoa ushuru.
Kumbe unawajibika “kurudisha” yaani kulipa kodi kwa sababu unalo deni kwa serikali
inayokuhudumia. Nikifikiria kile ambacho nimepokea, katika uwanja wa elimu, wa afya,
na mambo gani nimewahi kupata bure, kadhalika nimepata zaidi ya kile ninachoweza kutoa.
Kadhalika
ninalo deni kubwa kwa wazazi, kwa marafiki, kwa walimu, kwa yule aliyenifundisha imani,
kwa aliyenipa upendo, kwa wale wanaoleta maendeleo, ama kweli mimi nimebaki kuwa kama
kipande tu cha madeni. Haitoshi tu kuuliza: eti wewe unafikiri nini juu ya nchi yetu?
Bali yatakiwa kuuliza: wewe utairudishia kitu gani jamii yetu?
Unafanya nini
ili kuninusuru nchi yetu na ubadhilifu na rushwa, na uonezi na magomvi. Ushirikiano
wa kwanza ni ule wa kulipa kodi. Kwa kufanya hivyo, utawafundisha hata wale wajeuri
wengine wanaodanganya jamii na kunyonya taifa na kuwanyonya wanyonge.
Swali
zito kwa mkristu lingekuwa ni namna gani mmoja anaweza kumrudishia au kumpa kodi Kaisari
mkoloni (mbaya) au Kiongozi fisadi (yaani viongozi wevi na wachakachuaji) ambao sina
imani nao kabisa. Yaani kulipa kodi kwa serikali badhilifu. Katika hali kama hiyo
ndipo inapoingia sifa ya Yesu, ya kutokutazama uso wa yeyote, kama walivyosema wapinzani
wake: “twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na hutazami sura za watu.”
Kwa
hiyo, kuwajibika kwa Kaisari au viongozi fisadi wanaoiba maana yake ni kumpa kodi
au ushuru wake, yaani kumpa ukweli anaostahili, kumpa ile sauti ya ukweli na uwazi
itakayomkereketa dhamiri na kumwajibisha ili awe mtu wa kutenda haki. Kama jinsi vyombo
vya habari, au vyama mbalimbali vya kisiasa na dini vinavyoikosoa serikali ili ovyo.
Huo ndiyo ushuru na kodi ninayowajibika kumlipa Kaisari au kiongozi mbadhilifu.
Kwa hiyo dini haiingilii mambo ya serikali na siasa bali sehemu ya wajibu wake kwa
Kaisari.
Baada ya kuwajibika hivyo kwa Kaisari, kwa serikali na kwa viongozi,
kunafuata kuwajibika kwa Mungu. Mpe Mungu yaliyo ya Mungu. Mosi, sisi binadamu tumeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu. Sisi ni tuko kama sanamu, picha, sura ya Mungu. Kumrudishia
Mungu yaliyo yake, maana yake tuoneshe kama kweli kuwa tu hiyo picha ya Mungu wa amani,
wa haki na upendo kwa wote. Kama vile tunavyosafisha picha zetu zinapokuwa na vumbi,
ndivyo nasi tujikosoe na kujisafisha tuwe safi dhidi ya uovu ili daima tuakisi uzuri
wa Mungu ulio ndani yetu.
Pili, Wafarisayo walikuwa wanatunza mifukoni mwao
pesa ya Kaisari, na wanaambiwa wamrudishie pesa yake. Kadhalika yaonekana wameshikilia
pia kwa namna isiyo sawa mali, mamlaka, na haki za Mungu, basi wanaambiwa mamlaka,
na mali zote ni haki ya Mungu, basi wamrudishie. Wamwachie Mungu kupata heshima yake
Mungu wasimpore heshima yake.
Kwa lugha hiyo, Yesu alitaka kumpokonya au kumvua
Kaisari cheo cha kimungu, na kutenganisha kabisa vyeo hivi, na “kumwacha Kaisari aitwe
biandamu na Mungu aitwe Mungu” Kwa hiyo, “Kumpa Mungu yaliyo ya Mungu” maana yake
Kaisari apewe vitu, lakini Mungu apate watu, nafsi na heshima yake yote, na ukuu wake
wote, dhamiri yake, moyo wake.
Kwangu Yesu anasema: usiandike kitu kingine
moyoni mwako zaidi ya Mungu. Uwe huru na aina yoyote ile ya mawazo, makusudio, usitawaliwe
na chochote; uyakatalie mamlaka hayo hayakuhusu. Kwa kila mamlaka ya kibinadamu Yesu
anasema: Usimtawale binadamu, usitawale dhamiri ya binadamu. Binadamu anamhusu Mungu,
ni kitu au nafsi ya Mungu. Mtu anaye Mungu katika damu. “Mwache Kaisari awe Kaisari
na Mungu aitwe Mungu.”