Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa
Karibuni mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican tusafiri pamoja katika kuumega mkate,
ndiyo Neno la Mungu, chakula cha roho zetu. Ni Dominika ya 29 ya mwaka A wa Kanisa.
Mpendwa, ujumbe wa tafakari yetu ni utambuzi wa namna gani mwamini mkristu aweze kuishi
ukristu wake katika maisha ya kawaida ya kijamii, akishiriki mambo yote bila kuharibu
mpango wa Mungu, na hivi kumbe kuingiza daima chachu ya Injili katika maisha ya kidunia.
Katika somo
la kwanza tunamwona nabii Isaya akitafakari mpango wa Mungu ulio wa ajabu. Wakati
Waisraeli wamekata tamaa, Mungu anamtuma mfalme mpagani wa Persia yaani Koreshi ambaye
ataiteka Babilonia na baadaye atawaweka huru Waisraeli warudi nyumbani. Ataruhusu
tena mahekalu yaliyobomolewa na Wababilonia yajengwe na kila mmoja ataruhusiwa kushiriki
dini yake katika uhuru.
Nabii Isaya anatafsiri hali hii, kuwa ni mpango wa
Mungu wa wokovu kwa taifa la Israeli. Anamwona huyu Koreshi kama mchungaji, mtu aliyeletwa
na Mungu, mpendwa wa Mungu. Anaonekana kama masiha lakini nabii Isaya haoneshi kuwa
yeye ndiye mfalme wa Israeli atakayekuja kwa ajili ya ukombozi wa Israeli. Ni chombo
cha Mungu kwa kuondolewa utumwani huko Babeli.
Mpendwa, mara kadhaa tuko utumwani
hapa nchini petu, kijijini petu, je tunaona alama za nyakati ambazo Mungu huweka katikati
yetu akituonesha kuwa yu pamoja nasi katika shida zetu na hivi katika yeye twaweza
kuondolewa katika shida hizo? Ninachotaka kukuambia ni hiki, kuza moyo na macho yako
ili daima uone mpango wa Mungu maishani mwako kila siku katika kile tunachokiita alama
za nyakati!
Mpendwa msikilizaji, ni kwa njia ya sala na kuombeana kijumuiya
twaweza pia kuona mpango wa Mungu. Si sala na maombi tu bali kurutubisha na kudumu
katika imani tuliyoipokea wakati wa ubatizo kwa majitoleo mengine yampendezayo Mungu.
Jambo hili linasisitizwa na Mtume Paulo kwa Watesalonike akiwaambia kuwa anawakumbuka
kwa sala na kuwapongeza kwa maana kile alicho kisia kinakua na kuzaa matunda ndiyo
upendo na moyo wa kuikuza imani katika Yesu Kristu na sasa anataka wadumu katika imani
bila kurudi nyuma.
Katika Injili ya leo kutoka mwinjili Mathayo tunajifunza
kuwa Imani ni jambo ambalo hatuwezi kuliishi nje ya dunia hii, yaani bila uhusiano
na shughuli za kijamii. Mtu aliye mkristu anaishi katika jamii ya watu. Imani si jambo
la siri wala la muda mfupi bali ni jambo la wazi kabisa na la muda wote. Ni kwa jinsi
hii dini hujikita katika maisha ya kawaida ya kijamii na kisiasa na humdai mtu kushiriki
kazi zote za kijamii. Kila Mkristu yampasa kuchangia maendeleo ya mwanadamu na jamii
kwa ujumla na zaidi kuwa mfano bora kwa wengine.
Katika Injili ya Dominika
hii ya 29 kielelezo msingi cha kuwajibika kijamii kinatujia kwa sura ya kodi kwa Kaisari.
Kumbe ni vema na ni lazima na muhimu kulipa kodi au tuseme kuwapo pamoja na wengine
katika kusimamia mambo yahusuyo haki na amani katika jumuiya, lakini pia tunao wajibu
wa kuhoji hiyo kodi inatumikaje na hivi kusukuma mbele lengo lake liweze kufikiwa
bila kuharibu utulivu wa jamii husika. Ndiyo kusema tunapaswa kuingiza chachu ya Injili
katika maisha ya jamii (Rejea Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, GS)
Tunapozungumza
ya Mungu mpe Mungu tunataka kusema yale yote ambayo ametuagiza tuyafanye kwa sifa
na utukufu wake lazima tuyafanye kwa unyenyekevu, kwa upendo na ufasaha. Injili inatupa
fundisho zuri kweli nalo ni hili: mpende Mungu kwa akili yako yote, kwa moyo wako
wote na kwa roho yako yote na kisha jirani yako!
Jirani ni mwanadamu mwenzako
ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huyu jirani ndiye unapaswa kumrudishia
Mungu, ndiyo yaliyo ya Mungu. Jirani huyu ndiye ambaye unakutana naye ofisini, katika
siasa na katika familia. Kumbe, tengeneza maisha ya kijamii yaliyo mazuri na hivi
mwanadamu atainuliwa juu katika utu wake na Mungu ataisifiwa katika mwanadamu huyu
na hivi wajibu wako wa kumpa Kaisari yaliyo yake na Mungu yaliyo yake utakuwa si wajibu
pinzani bali wajibu mwafaka kwa wokovu wako.
Fundisho hili latupa changamoto
ya kuheshimu wanadamu wote na hivi polepole kukua katika kutambua chanzo chao ambacho
ni Mungu. Viongozi wote wa uma kumbukeni wajibu huu daima ili kusudi kazi ya kuongoza
isiwe chanzo cha kupotea bali utumishi mtakatifu utakaokuletea wokovu.
Tumsifu
Yesu Kristu na Maria. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.