2014-10-16 08:20:10

Mchango wa Paulo VI katika Mafundisho Jamii ya Kanisa!


Mtumishi wa Mungu Giovanni Battista Montini alizaliwa mnamo tarehe 26 Septemba 1897 huko Brescia kaskazini mwa italia. Siku ya kuzaliwa kwake alionekana kuwa dhaifu sana kiafya, jambo lililo wafanya wakunga waliokuwa wanamsadia mama yake kujifungua kusema kwamba, mtoto yule angeishi kwa siku moja tu! Alichaguliwa kuliongoza Kanisa kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII, ambaye kwa sasa ni Mtakatifu kilichotokea tarehe 3 Juni 1963. Montini aliliongoza Kanisa kuanzia tarehe 30 Juni 1963 hadi tarehe 6 Agosti 1978 kwa jina la Papa Paulo VI. RealAudioMP3

Mchango wa Papa Paulo VI unaonekana sana katika mafundisho yake kuhusu jamii yaliyomo kwenye waraka ” Populorum Progressio” au Maendeleo ya watu”, ambamo anasisitiza kuwepo uwiano kati ya imani ya kikristo na haki ya kupata maendeleo ya kiuchumi kwa kila taifa na kwa kila mtu. Katika kuzungumzia maendeleo ya watu “Populorum Progressio”, Papa Paulo VI anatumia neno “maendeleo” jinsi linavyo eleweka kijamii na kiuchumi, na anajaribu kulioanisha na uelewa wa kikristo juu ya mwanadamu na jumuiya anaomoishi.

Ana sisitiza kwamba, maendeleo ya watu, na kwa namna ya pekee, hasa maendeleo ya wale wanao pambana ili kujikomboa kutoka kwenye baa la njaa, maradhi na ukosefu wa Elimu; wale wanao pambana ili kuweza kupata haki zao msingi katika kushiriki utajiri ambao Mwenyezi Mungu ameikirimia dunia kwa manufaa ya wote, ni sehemu ya utume na maisha ya Kanisa.

Barua hii ilitolewa kwenye takriban miaka miwili baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kipindi ambacho dunia katika ujumla wake ilikuwa kwenye shamrashamra za aina mbalimbali. Itakumbukwa kwamba, katika kipindi hiki, nchi nying za Afrika zilikuwa zikijipatia uhuru wa bendera. Kulikuwa pia na mabadiliko mengi duniani kiuchumi, kisiasa na kijamii. Maendeleo ya sayansi na teknolojia za mawasiliano yalikuwa yakikua kwa kasi, kiasi cha Umoja wa mataifa kutangaza kwamba kipindi chote cha kuanzia mwaka 1960 kilikuwa ni kipindi cha maendeleo ( “Decade of Development”). Si hayo tu, bali pia uchumi ulikuwa unakua kwa kasi pamoja na ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi mbalimbali duniani, jambo ambalo lilionekana kama ndoto katika historia ya binadamu. Lakini pamoja na maendeleo hayo, kulikuwa na tofauti kubwa za kiuchumi na kimaisha kati ya watu na watu na kati ya mataifa.

Itakumbukwa kwamba dunia bado ilikuwa imegawayika katika makundi matatu, au dunia tatu kama inavyojukana. Dunia ya kwanza ilikuwa inajumuisha nchi za magharibi mwa ulaya pamoja na marekani, dunia ya pili ikajumuisha nchi za Ulaya ya mashariki, yaani nci za kikomunisti pamoja na China, na dunia ya tatu ilijumuisha nchi za Afrika, Asia na Amerika ya kusini, ambazo ziliitwa Nchi maskini na zinazo anza kujipatia maendeleo. Katika ziara zake za kichungaji Amerika ya kusini na Afrika, Papa Paulo VI aliweza kujionea mwenyewe umaskini wa hali na mali uliokuwa unawakumba watu wa maeneo aliyotembelea. Hivyo basi, Waraka wake huu Populorum Progressio una pata chimbuko lake katika uhalisia wa maisha ya watu, na ndiyo maana anasisitiza kwamba, maendeleo yapanie kumsaidia mtu mzima kiroho na kimwili.

Hivyo basi, mchango wa Papa Paulo VI katika mafundisho jamii ya kanisa unaonekana katika msisitizo alio toa kwamba: maendeleo ya kweli ni yale yanayo muwezesha mwanadamu kujikomboa kutoka katika hali ya umaskini na kumuweka katika hali ya kuweza kujipatia yeye mwenyewe mahitaji yake yote kwa njia ya kufanya kazi. Hii ina maanisha kwamba watu wakipewa fursa ya kujiendeleza na kuondokana na umaskini wataweza kuondokana na hali ya kuishi kwa hofu na kuwa wawajibikaji katika maisha bila kujisikia kukandamizwa katika jamii. Maendeleo yanayo gusa utu wa mtu kiroho, kimwili, kiakili na kimahusiano na kimakuzi katika jamii yake ndiyo ambayo yanaweza kuuthamini utu wa mtu.

Licha ya maendeleo yaliyoletwa na sayansi na teknolojia za mawasiliano na vyombo vya usafiri, Papa Paulo VI alionya pia kuhusu hatari ya kusambaratika kwa mila na desturi njema za watu kutokana na uelewa hasi wa maendeleo. Ilionekana kwamba, kabla ya utandawazi jamii nyingi zilithamini imani, familia, ushirikiano katika jamii, heshima kwa watu walio pewa dhamana ya kuongoza jamii na dini za watu. Ila katika ulimwengu ambao unajiita wa kisasa, mambo yote haya yanaonekana kama kikwazo cha maendeleo, kutokana na tasfiri isiyo sahihih kuhusu maendeleo. Katika hali hii Papa Paulo VI ana waalika watu watafakari maana ya maendeleo, ambayo kwake yeye si maendeleo ya vitu bali ni maendeleo ya watu bila kusahau mila na desturi zao njema.

Kwa wale wanaoungama imani ya kikristo, Papa Paulo VI ana sisitiza kwamba, maendeleo yaeleweke kupitia imani wanayoiungama, kwani hakuna maendeleo yoyote yanaweza kupatikana katika kumtenga mwanadamu au mkristo na imani yake, na hata kwa wale wasio ungama imani yoyote, maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana katika kumtenganisha mwanadamu na mila na desturi zake au na uchumi wenyewe. Yaani, uchumi ni kwa ajili ya mwanadamu na si vinginevyo.

Mambo yanapokwenda kinyume na hapo, matokeo yake ni ukosefu wa haki kati ya watu na watu na pia kati ya mataifa. Ndiyo maana papa Paoulo VI ana sisitiza kwamba, maendeleo yaliyo ya kweli yanaleta haki na amani katika jamii na kati ya mataifa, na kwamba mahali ambapo haki inakosekana, hapawezi kuwa na maendeleo wala amani. Hivyo basi, maendeleo ni namna ya kuleta haki na amani katika jamii yoyote ile.

Makala haya yameandaliwa na
Rev. Dr. Sr. Gisela Upendo Msuya, mtaalam wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, Angelicum, Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.