Baada ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia iliyokuwa inafanyika
katika makundi madogo madogo katika vikao vyake saba, Alhamisi tarehe 16 Oktoba 2014,
Mababa wa Sinodi wamepokea taarifa za vikundi na kuanza kuifanyia kazi kwa kusikiliza
mchango kutoka kwa Mababa wa Sinodi.
Mchango wa makundi baada ya kukamilika,
utakuwa ndio matunda ya kazi ya Mababa wa Sinodi, inayojulikana kwa lugha ya Kilatini
"Relatio Synodi" kama alivyobainisha Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican
wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican kuhusiana na Sinodi.
Hati ya Mababa wa Sinodi itawakilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe
18 Oktoba, tayari kufanyiwa kazi.
Kardinali Lluis Martines Sistach anasema,
majadiliano kwenye makundi yamefanyika katika misingi ya umoja na mshikamano; udugu
pamoja na kuzingatia changamoto za kichungaji. Mababa wa Sinodi wameonesha uhuru na
ukomavu, ukweli na uwazi katika kujadili hata zile mada tete, kwa kutambua kwamba,
kuna changamoto za kichungaji zilizoko mbele yao zinazopaswa kufanyiwa kazi.
Kardinali
Joseph Edward Kurtz kwa upande wake anasema, Mababa wa Sinodi wamezungumza kwa uhuru
wakiwa na nia moja katika majadiliano, kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kuliwezesha
Kanisa kutoa mwelekeo chanya wa kimissionari na ujumbe wa matumaini pasi na kukata
wala kujikatia tamaa.
Askofu mkuu Rino Fisichella anasema, matatizo na changamoto
za kifamilia ni kielelezo cha mtikisiko wa imani, pale ambapo familia zinajikita katika
imani thabiti, hapo hakuna cheche za kinzani katika tunu msingi za maisha ya ndoa
na familia.