2014-10-15 07:54:17

Watu wanakufa kwa baa la njaa, lakini bado kuna watu wanachezea chakula duniani!


Jumuiya ya Kimataifa tarehe 16 Oktoba 2014 inaadhimisha Siku ya Chakula Duniani huku kukiwa na changamoto kwa watu kubadilisha mtindo wa maisha ili kuokoa chakula kingi kinachotupwa kila mwaka. Utafiti uliofanywa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, chakula kinachotupwa kila mwaka kina kadiriwa kuwa na thamani zaidi ya Euro Billioni elfu mbili.

FAO inabainisha kwamba, bado kuna gharama kubwa kutokana na matumizi mabaya ya chakula duniani, kwani hapa pia kuna uharibifu na uchafuzi mkubwa wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, kinzani na chokochoko za kisiasa na kijamii sanjari na ubadhirifu wa fedha ya umma kwa ajili ya kugharimia sera na mikakati ya kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa chakula ambacho kamwe hakitaweza kuwafikia walaji.

FAO inasema kwa hakika kwamba, kuna matumizi mabaya ya chakula duniani, hususan katika nchi zilizoendelea zaidi duniani, kwani inakadiriwa kwamba, asilimia 36% ya chakula chote kinachozalishwa duniani kinaishia kwenye mashimo na mapipa ya taka! Kumbe, mchakato wa kupambana na matumizi mabaya ya chakula ni sehemu ya mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na baa la njaa duniani.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna watu duniani wanakula na kusaza, lakini upande mwingine wa dunia kuna watu wanakufa kwa njaa na utapiamlo pamoja na maradhi. Kutokana na changamoto hizi, FAO pamoja na Shirika la Afya Duniani, WHO, wameamua kwa pamoja kulivalia njuga baa la njaa na utapiamlo kwa kuimarisha mikakati ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula bora duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.