2014-10-15 15:29:45

Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, majadiliano ya vikundi yanaendelea!


Mababa wa Sinodi, Jumatatu tarehe 13 Oktoba 2014 walipokea hati elekezi, muhtasari wa tafakari na mchango uliotolewa na Mababa wa Sinodi wakati wa maadhimisho ya Sinodi katika juma la kwanza. Hati hii imeendelea kuchambuliwa na Mababa wa Sinodi katika makundi madogo madogo, ili hatimaye, kuweza kutoa hati ambayo itawakilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, ili aweze kuifanyia kazi, mintarafu maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 Hadi tarehe 25 Oktoba 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari, siku ya Jumanne, tarehe 14 Oktoba 2014, Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican alionesha masikitiko yake kutokana na tafsiri finyu iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kiasi hata cha kupotosha ujumbe uliotolewa na Mababa wa Sinodi katika hati yao elekezi. Mkutano na waandishi wa habari umehudhuriwa pia na Kardinali Fernando Filoni pamoja na Kardinali Fox Napier kutoka Afrika ya Kusini.

Mchango unaotolewa na Mababa wa Sinodi utawasilishwa kwenye kikao cha Sinodi, Alhamisi asubuhi, tarehe 16 Oktoba 2014 na hapo hati ya Mababa wa Sinodi inatarajiwa kutangazwa rasmi baada ya majadiliano ya Mababa wa Sinodi katika makundi. Hii hati inajulikana kama "Relatio Synod" ndiyo ambayo itakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu, tayari kuifanyia kazi kama matunda ya sala na tafakari kutoka kwa Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia.

Makardinali hawa wakizungumza na waandishi wa habari wanasema kwamba, majadiliano yanaendelea na kwamba, Mababa wa Sinodi wanaendelea pia kutoa mapendekezo na ushauri wao katika tema mbali mbali zilizokwisha kujadiliwa, ili kutoa hati makini kwa Baba Mtakatifu kwa ajili ya maadhimisho ya awamu ya pili ya Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2015.







All the contents on this site are copyrighted ©.