Jumuiya ya Kimataifa, Jumatano tarehe 15 Oktoba 2014 inaadhimisha Siku ya Kunawa Mikono
Kimtaifa, changamoto iliyotolewa na Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa,
UNICEF, ili kuokoa maisha ya watoto chini ya miaka mitano wanaofariki dunia kutokana
na magonjwa ya kuhara.
UNICEF inasema magonjwa ya kuhara kwa watoto ni chanzo
kikubwa kwa watoto hao kudumaa, mambo yanayosababisha madhara makubwa kwa ustawi na
maendeleo ya kiuchumi. Tabia na utamaduni wa kunawa mikono kila wakati ni mchakato
unaoweza kuwakinga watoto wadogo dhidi ya magonjwa ya kuhara.
Ni kitendo cha
kawaida kabisa kunawa mikono kwa sabuni, lakini kina maana kubwa kwani kinaweza kuokoa
maisha ya watoto ambao ni tegemeo kubwa la taifa. Watoto wadogo waelimishwe umuhimu
wa kunawa mikono kabla na baada ya kula na wakati wote wanapomaliza kujisaidia. Watoto
wakijengewa tabia ya kunawa mikono, wataweza kuimarisha afya zao kwa kujikinga na
magonjwa ya kuhara ambayo yamekuwa ni chanzo kikubwa cha vifo vingi vya watoto duniani.