2014-10-15 11:34:37

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere!


Miaka 15 imekwishagota tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania alipofariki dunia. Watanzania wanahamasishwa kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa kujikita katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kutambua kwamba, uhuru wa watanzania unawachangamotisha kujitegemea. RealAudioMP3

Mwalimu Nyerere alijipambanua kitaifa na kimataifa kama kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, changamoto endelevu kwa watanzania wakati huu wanapoendelea kumuenzi. Mwalimu alitaka kuona Tanzania inakuwa na siasa safi na uongozi bora kwani kwake uongozi ulikuwa ni kielelezo cha huduma.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akiwa mjini Vatican katika Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia anabainisha mchango uliotolewa na Mwalimu Nyerere katika kupigania uhuru, haki, umoja na mshikamano wa kitaifa. Ni kiongozi aliyependa kuona watanzania wengi wanashiriki katika ustawi na maendeleo ya nchi yao kwa kudumisha utawala bora.

Askofu Ngalalekumtwa anasema mchakato wa Mtumishi wa Mungu Mwalim Nyerere kutangazwa kuwa Mwenyeheri unaendelea na kwa sasa bado uko katika ngazi ya Kijimbo. Anamwombea kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kumtakasa na hatimaye, kumkaribisha katika makao ya wenye haki mbinguni.







All the contents on this site are copyrighted ©.