Shirika la Afya Duniani, WHO, linasema kwamba, kasi ya maambukizo ya ugonjwa wa Ebola
huko Afrika Magharibi inaweza kuongezeka maradufu hadi kufikia wagonjwa 10, 000 kwa
juma katika kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa. Ugonjwa huu umekwisha sababisha
vifo vya watu 4, 500 wengi wao wakiwa ni wagonjwa kutoka Afrika Magharibi.
Hii
ni changamoto kubwa ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na Umoja wa Mataifa kabla mambo
hayajaharibika zaidi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo walau vijana 7, 000
kwa ajili ya kutolea tiba kwa wagonjwa na kikosi kazi cha watu 500 kitakachoshughulikia
maziko ya wagonjwa watakaofariki kwa Ebola. Rais Barack Obama wa Marekani akizungumza
na viongozi wa kijeshi kutoka Marekani na Washirika wake amebainisha kwamba, Jumuiya
ya Kimataifa bado haijauvalia njuga ugonjwa wa Ebola.
Wakari huo huo, Serikali
ya Uingereza imetuma Meli ya Kijeshi ikiwa imesheheni watu 400 kati yao wakiwa ni
wanajeshi, waganga na wauguzi kwenda Siera Leone ili kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa
wa Ebola nchini humo. Liberia na Guinea ni kati ya nchi za Afrika magharibi zilizoathirika
zaidi kwa ugonjwa wa Ebola.