2014-10-15 16:12:51

Jiwekeni tayari kwa ujio wa Bwana..


Katika Nyakati za Mwisho itakuwaje kwa watu wa Mungu? Ni nini kitakacho tokea kwa kila mmoja wetu? Na sasa tufanye nini? Ni maswali aliyouliza Baba Mtakatifu Francisko, mwanzo wa mafundisho yake kwa mahujaji na wageni kwa Jumatano hii. Katika katekezi hii ameendelea na mfululizo wa tafakari juu ya Kanisa la Kristo, leo akilenga zaidi ujio wa pili wa Bwana. Amesema ni kusubiri kwa hamu kubwa, kama Bibi harusi anavyosubiri ujio wa Bwana harusi wake.

Papa alirejea maelezo ya Mtume Paulo, kwa Wakristo wa Thesalonike, ambao pia waliulizana maswali kama haya, wakisubiri kwa hamu kuuona ujio wa Bwana. Mtume Paulo aliwaambia, "Kisha sisi tulio hai , tuliosalia ,tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani, na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana Milele ,basi farijianeni kwa maneno hayo" (1 Wathesalonike 4:17).

Maelezo ya Papa, pia yalirejea ishara mbalimbali zilizoandikwa katika Kitabu Kitakatifu cha Bibilia , kama ilivyokitabu cha ufunuo wa Yohana, au kama yaliyo maono ya Manabii, yanavyo elezea juu ya mwelekeo wa mwisho, hatimaye, katika mji mpya wa Yerusalemu, ulioonekana ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni, tayari kama bibi arusi aliyekwisha kupambwa kwa ajili ya mumewe (Ufunuo 21,2). Katika haya Papa alitoa ufafanuzi kwamba, ni Kanisa, ambao ni watu wa Mungu, wanao fuatana na Bwana Yesu, huandaa pamoja naye mipango yao ya siku hadi siku, kama vile bibi anavyo jiandaa kukutana na bwana harusi wake.

Papa anasema, si tu suala la kusema, lakini kweli itakuwa kweli siku ya kushereheka, Siku ya harusi! Kwa sababu Kristo, katika kuwa binadamu kama sisi, alitufanya sisi sote kuwa wamoja pamoja naye, katika kifo chake na ufufuo wake. Anakuwa kweli bwana harusi na sisi ni bibi harusi wake. Ujumbe huu ni mzuri zaidi katika ukamilifu wa mpango wa ushirika na upendo wa Mungu katika historia ya binadamu.

Aidha Papa amezungumzia kipengele kingine, kinachotoa faraja kwa Wakristo kwamba, ni kuufungua moyo, kama Mwinjilisti Yohana anavyo andika kwamba, katika Kanisa, bibi harusi wa Kristo, mnaonekana mji mpya “Yerusalemu mpya". Hii ina maana kwamba Kanisa, kama vile bibi, linaitwa kuwa mji, ishara ya maisha ya pamoja, umoja na mshikamano katika uhusiano wa binadamu. Basi kwa jinsi inavyokuwa vizuri kutafakari hali ya mwisho, kama pia inavyoonyesha katika ishara nyingine katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana, watu wote na mataifa yote wamekusanyika katika mji huu, kama katika hema, "Hema la Mungu" (Ufu 21: 3)! Na katika sura hii kutakuwa na utukufu zaidi na hapatakuwa na kutengwa, wala uonevu wala ubaguzi wa aina yoyote - iwe kijamii, kikabila au kidini - lakini sisi wote tutakuwa wamoja katika Kristo.

Papa amelitaja tukio hili kuwa ni nzuri katika uzuri wote, tunao weza kuona katika tumaini la Kikristo. Na roho zetu haziwezi kukoma katika kuwa na hamu na matumaini ya kuisubiri Siku hii kwa shauku kubwa, Siku ya kutimia kwa siri, siri ya upendo wa Mungu ambamo wafuasi wa Kristo , watazaliwa tena upya na kuishi milele. Ni tukio la kusubiri mtu aliyembali lakini pia yu karibu nasi, ambaye ndiye Kristo Bwana. Kanisa basi lina kazi ya kuwasha taa na kuiweka mahali pa wazi kwa ajili ya kumlikia matumaini haya na kuendelea kuangaza kama ishara ya uhakika wa wokovu. Mwanga unaoangazia ubinadamu wote, katika njia inaongoza katika kukutana na sura yenye huruma ya Mungu.

Papa alikamilisha Katekesi na mwaliko kwa watu wote wake kwa waume, kwamba hakuna cha kusubiri, wakati ni huu wa kujiandaa kwa ajili ya kumpokea Bwana Harusi. Kanisa kwa hamu linamsubiri Bwana Harusi wake. Na hivyo ni lazima tujiandae vyema, tuwe safi , na mashahidi wa kweli wa tumaini hili. Kuna wengi ambao wameshikwa na uchovu katika kumsubiri Bwana wa wokovu, na sisi tunapaswa kuwatia nguvu mpya, na kuwainua, na kuwasaidia kuziwasha taa zao tayari kwa ujio wa Bwana Harusi. Ni kuhakikisha tuna mafuta ya kutosha ya imani. Papa alieleza na kuomba msaada wa Mama Bikira Maria, Mama wa Matumaini na Malkia wa Mbingu, atutie nguvu daima wakati tunaposubiri kurejea kwa Bwana Harusi. Kusubiri katika usharika na umoja na muungano kamili wa kiroho.








All the contents on this site are copyrighted ©.