Changamoto za kichungaji katika maisha ya ndoa na familia!
Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia wanakiri kwamba kuna matatizo makubwa,
changamoto na fursa mbali mbali katika kutangaza Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa.
Mababa wa Sinodi wamekumbusha kwamba, Kanisa ni nyumba inayopaswa kuwakaribisha watu
wote hata wale wanaoishi katika mwelekeo wa ndoa za jinsia moja bila kuhatarisha mafundisho
tanzu ya Kanisa Katoliki kuhusu ndoa na familia.
Ieleweke kwamba, Kanisa halijaruhusu
wala kuridhia ndoa za watu wa jinsia moja kama inavyosomeka kwenye vyombo mbali mbali
vya habari!
Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Nigeria katika mahojiano maalum na Radio Vatican anafafanua kwamba, changamoto kubwa
kwa Kanisa Barani Afrika ni ndoa za wake wengi, ndoa za mseto, umaskini, ukosefu wa
fursa za ajira kwa vijana. Pale ambapo kuna msingi thabiti wa ndoa, hapo familia inakuwa
kweli ni chombo cha ushuhuda wa imani tendaji na sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji
mpya.
Askofu Kaigama anasema, ndoa za wake wengi ni changamoto kubwa ya kichungaji
kwa Kanisa Barani Afrika. Kuna baadhi ya watu wanatamani kuwa kweli ni waamini wa
Kanisa Katoliki, lakini wanajikuta wakiwa na kikwazo hiki cha wake wengi. Ndiyo maana
kwa hekima na busara Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu wanayaalika Makanisa mahalia
kuendeleza majadiliano ya kina yatakayowawezesha Mababa wa Sinodi kuibuka na mbinu
mkakati wa kichungaji wakati wa maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu
kuhusu Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba
2015.
Ndoa za mseto ni changamoto nyingine hasa pale inaposhikamanishwa na
misimamo mikali ya kiimani kama inavyojionesha nchini Nigeria ambako Kikundi cha Boko
Haram kinataka kuwasilimisha wananchi wote wa Nigeria ili wawe ni waamini wa dini
ya Kiislam, jambo ambalo linakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Boko Haram
ni tishio kwa maisha, usalama na ustawi watu: kiroho na kimwili.