2014-10-14 16:00:34

Papa: hakuna imani " vipodozi", bali ni kutenda kwa upendo


Baba Mtakatifu Francisko katika Mahubiri yake mapema Jumanne hii katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta alihoji iwapo imani na maisha yetu ya Kikristo, ni maisha ya kujipendekeza na kujionyesha tu kama mapambo na kumbe ndani mwake hakuna imani hai katika upendo wa Kristo. Imani, Papa alisema, si tu katika kuwa watu wa sala na kumkiri Mungu, ila ni kuchagua kuachana na maovu, uchoyo na tamaa za kidunia. Imani ya kweli ni maisha ya majitolea ya sadaka kwa ajili ya wengine, hasa maskini.

Imani haina haja ya kujionyesha, ila ni utendaji halisi. Haina haja ya kuwa mfungwa wa upendo wa kinafiki, iwapo moyo hauna upendo wa kweli. Papa Francisko alieleza, akiirejea Injili ya siku, ambamo Mafarisayo wanashangazwa na Mafundisho ya Yesu juu ya sheria ya kunawa kabla ya kula. Yesu alirudia kukemea unafiki wa kuwaweka wengine hatiani kwa sababu hawajatimiza kikamilifu sheria.

Papa alifafanua kwamba, Yesu alilaani vikali roho hii ya kujipamba kwa nje, na kuonekana mzuri , lakini kumbe ndani ni mtu mwingine! Alisema, Yesu analaani watu wanaotembea katika tabia hii ya unafiki wa kujipamba kwa nje lakini kumbe ndani wana tabia mbaya, tabia ya kufanya mambo mabaya kisirisiri bila ya kuonekana. Kujionyesha kama ni watu wa haki , watu wa ibada , wanaotembea mitaani wakisali, kufunga na kutoa msaada, lakini kumbe ndani mwao wamejaa udhalimu na uovu.

Yesu aliwafananisha watu hao na makaburi yaliyopakaliwa chokaa nyeupe ya kupendeza kwa nje na kumbe ndani mwake mmevunda kwa uozo , kama ilivyoandikwa katika Injili ya Mathayo. Yesu anayoonyesha kukerwa na mtu wenye tabia mbili zinazopingana, wema na uozo. Hata Paulo, katika waraka wake kwa Wagalatia, amezungumzia tabia ya kujishikamanisha na sheria kwa nje na kisiri kuwa na utendaji tofauti.
Papa Francisco alisisitiza kwa sababu hiyo, kuzishika sheria peke bila matendo hakuwezi kutuokoa. Jambo la maana zaidi ni kuwa na imani, yenye kutoa jibu katika njia ya upendo. Na ndivyo Yesu alivyowaambia Mafarisayo, kwamba, imani si tu kuzisoma sheria na kuzikariri. Aliongeza, “Sisi wote tunaamini katika Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, uzima wa milele. ... Sisi wote ni wanaamini! Lakini imani isiyo na upendo kwa mtu mwingine, ni imani iliyokufa. Yesu Kristo anatuhimiza kuwa na imani inayojibidisha katika utendaji unaotokana upendo kwa ajili ya mwingine, ni kufanya kazi zetu za kila siku si kwa manufaa yetu wenyewe lakini hasa kwa manufaa ya jirani na watu wengine hasa wanaohitaji huduma tulizo dhaminishwa. Na si kuwabebesha wengine sheria nzito ambazo sisi wenyewe hata sisi wenyewe hatuwezi kuzitimiza. Na imani ya kweli huonekana katika matendo si katika kutolea maombi au Mtu wa sala masaa yote. Imani ni zaidi ya kuomba na sala. Imani ni kuvunjilia mbali moyo wa udikteta wa fedha au kuhusudu fedha, na tamaa kwa munufaa binafisi na uchoyo, na kila jambo linalotuweka mbali na Yesu Kristo. "

Papa Francisko alieleza kwa kukumbuka Padre Arrupe, aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Wajesuits katika miaka ya sitini, ambaye siku moja, mwanamke tajiri alimkaribisha mahali pake kwa lengo la kumpa fedha kwa ajili ya safari ya utume nchini Japan, ambako alikuwa anakwenda. Mwanamke huyo alitoa bahasha yake mbele ya waandishi wa habari na wapiga picha. Padre Arrupe aliona mateso makubwa na kudhalilishwa.Lakini alivumilia kupigwa picha akipokea bahasha kutoka kwa mwanamke huyo mbele ya wapiga picha na wanahabari, kwa kuwa alihitaji fedha kwa ajili ya watu maskini wa Japan." Baadaye alipofungua bahasha, ndani ya bahasha hiiyo kulikuwa na dola kumi. Papa alihoji, je kitendo cha mwanamke huyo tajiri, hakikuwa cha kuupamba Ukristo wake kwa nje na ndani mwake ni makapi matupu? Je haya si maisha ya kuupamba Ukristo kwa vipodozi? Je huo ndiyo muonekano wa maisha ya imani kwa Kristo na imani hai katika upendo wake?

"Yesu anatushauri: kwanza tusipigie tarumbeta imani, na ushauri wa pili ni tusitoe msaada kwa vilivyo vya ziada. Bali tuwe kama yule mwanamke mzee, ambaye alitoa kila kitu alichokuwa nacho katika maisha yake. Yesu anamsifu mwanamke huyo mzee maskini kwa kutoa senti zake mbili za mwisho alizokuwa nazo. Aliitoa kidogo alichokuwa nacho kwa siri, labda kwa sababu alikuwa na aibu ya kutokuwa na uwezo wa kutoa zaidi, Papa alimalizia.








All the contents on this site are copyrighted ©.