"Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi wanaongezeka zaidi duniani"
Taarifa ya Benki ya Dunia inaonesha kwamba, kuna pengo kubwa kati ya watu wachache
wenye uwezo kiuchumi na kundi kubwa la maskini, "akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi",
hali inayotishia mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na baa la umaskini,
njaa na maradhi duniani. Taarifa inaonesha kwamba, ugonjwa wa Ebola kwa sasa ni tishio
kubwa kwa usalama wa maisha ya watu duniani, lakini pia hali ya uchumi si shwari sana
kwa mataifa mengi.
Benki ya Dunia inazitaka nchi wanachama kuandaa mbinu mkakati
utakaobainisha sera makini za kiuchumi zitakazosaidia kupambana na ongezeko kubwa
la maskini duniani. Viongozi wakuu wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa,
kwa pamoja wanasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa jibu makini litakalosaidia
kupambana na ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa ni tishio kubwa hata pengine kuliko ugonjwa
wa Ukimwi, bila ya kuzitenga nchi zile ambazo zimekumbwa na ugonjwa huu.
Wajumbe
wa mkutano mkuu wa Benki ya Dunia wameridhia kuanzishwa kwa mchakato wa kukusanya
fedha itakayosaidia kupunguza pengo kubwa kati ya matajiri na maskini pamoja na kupambana
na tatizo la ubaguzi. Ukosefu wa usawa katika masuala ya kijamii ni hatari kubwa kwa
maendeleo na ustawi wa Jamii husika. Changamoto hii haina budi kwenda sanjari na maboresho
ya huduma ya nishati, afya, maji safi na salama na elimu. Mwelekeo huu hauna budi
kujikita katika elimu na mabadiliko ya kijamii.