Waguswa na mahangaiko ya wanawake na wasichana huko Mashariki ya Kati!
Mashirika ya Wanawake Wakristo na Waislam kutoka nchini Australia, kwa pamoja yameguswa
na mahangaiko pamoja na mateso ya wanawake na wasichana walioko nchini Syria, Iraq
na baadhi ya nchi za Kiafrika. Vyama hivi vinalaani vitendo vinavyopelekea ubaguzi
wa kidini unaofanywa dhidi ya waamini wa dini mbali mbali duniani.
Kwa namna
ya pekee, wanasikitishwa na chuki na uhasama wa kidini wanaofanyiwa Wakristo huko
Mashariki ya Kati. Mashirika haya katika tamko lao, wanasema wameguswa na mahangaiko
ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupata
mafanikio ikiwa kama watu wataonesha moyo wa toba na huruma kwa kujikita katika hali
ya kuvumiliana na kusaidiana, huku wakitambua kwamba, tofauti zao za kidini ni utajiri
mkubwa na mpango wa Mungu kwa binadamu.
Mashirika haya yanawataka viongozi
wa kimataifa kuhakikisha kwamba, wanasaidia kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu
sanjari na uhuru wa kuabudu.