2014-10-13 14:29:39

Vijana wa kizazi kipya kushirikishwa mchango wa Mtumishi wa Mungu, Papa Paulo VI


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ijayo tarehe 19 Oktoba 2014 majira ya Saa 4: 30 asubuhi kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga rasmi awamu ya kwanza ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia sanjari na kumtangaza Mtumishi wa Mungu, Papa Paulo VI kuwa mwenyeheri. Hili ni tukio la neema na baraka kwa Mama Kanisa, ikizingatiwa kwamba, Papa Paulo VI alisimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Kutokana na umuhimu wa tukio hili katika maisha na utume wa Kanisa, Jimbo kuu la Roma limeandaa mkesha wa sala na tafakari utakaoongozwa na Kardinali Agostino Vallini kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sapienza, kilichoko mjini Roma. Mtumishi wa Mungu Giovanni Battista Montini, alikuwa na mchango wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwenye miaka 1960. Kardinali Vallini atawashirikisha vijana wa kizazi kipya mchango wa Papa Paulo VI, ikizingatiwa kwamba, Papa Paulo VI alikuwa ni kati ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sapienza kunako mwaka 1920 hadi mwaka 1922, wakati huo kilijulikana kama Chuo Kikuu cha Roma.

Takwimu zinaonesha kwamba, Papa Paulo VI alikuwa pia ni Padre mshauri wa maisha ya kiroho kwa Shirikisho la wanafunzi Wakatoliki Italia, kwa kifupi "FUCI" kuanzia mwaka 1923 hadi mwaka 1925. Kwa kuangalia mchango wa Papa Paulo VI katika maisha ya wasomi wengi, Jimbo kuu la Roma limeamua kuwashirikisha kwa namna ya pekee kabisa vijana wa kizazi kipya, ili kuonja matunda ya kazi na utume wa Papa Paulo VI katika maisha na utume wa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.







All the contents on this site are copyrighted ©.