2014-10-13 11:44:26

Timbwiri timbwiri za mnuso! Yaani we acha tu!


“Mnuso” ni utamu utokanao na kunusa harufu nzuri. Katika matumizi ya kiswahili cha mitaani neno hilo linamaanisha sikukuu au sherehe, nk. Mathalani sherehe za ndoa wanaita “Mnuso wa Arusi.”

Sifa ya kwanza ya mnuso wowote ule, ni kufurahi, kusherekea, kushangilia kwa kula na kunywa hata kucheza. Sifa ya pili ya mnuso ni kusherekea bure, yaani unaalikwa kufaidi bure, hakuna kudaiana michango wala kutoa zawadi. Unachotakiwa kuingia nacho kwenye mnuso ni nja na kiu yako, sanasana uwe tayari na furaha ya kujichana. Sifa ya tatu ya mnuso ni kupata fursa ya kusherekea pamoja na mwenye sikukuu, au na mgeni rasmi.

Masuala ya minuso ya arusi yalianza zamani sana hata kabla ya Yesu. Wakati wa Yesu watu walikuwa wanazungumza na kuotea ndoto juu ya mnuso wa bustani ya Edeni. Kwa vile watu walikuwa katika mzingira ya kuteseka, watu wakawa wanaotea ndoto ya kuwa na ulimwengu wa mnuso kama ule wa bustani ya Edeni, yaani ulimwengu wa Padadisi, kwa ajili ya watu wema ambao wanateseka. Ndoto aina hiyo inasimuliwa pia katika kitabu cha Nabii Isaya anaposema: “Bwana ataandaa karamu katika mlima Sion, karamu ya divai tamu, chakula”. Kwamba Mungu mwenyewe ataandaa mnuso. Marabi waliendelea kusema kwamba wakati huo utakapokuja, yaani mwisho wa dahari, watakatifu watakaa pamoja na Mungu na kila mmoja atasema: “Tazama huyu ndiye Mungu wetu.”

Msingi wa mahubiri ya Yesu ni kujenga ufalme wa Mungu, ambao katika injili ya leo tungeweza kuuita “Mnuso wa arusi”. Yesu mara nyingi anaanza mahubiri yake kwa kutangaza: “Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia” (Mk 1:15) toka hapo najiegemeza kwenye mifano mbalimbali anayotoa na ndivyo polepole anafunua “fumbo” la huo ufalme anaotaka kuujenga ulimwenguni.

Katika mandhali kama hii ya kitamaduni na ya kutaka kujenga “Ufalme wa Mungu” Yesu anatuletea mfano huu wa leo, wa baba mtu (mfalme) anayeandaa mnuso wa arusi kwa ajili ya mtoto wake. Yesu anaanza kusema: “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanae arusi.” Hapa Yesu anataka kuzungumzia juu ya karamu au sherehe za hapahapa duniani, tofauti na karamu waliyomaanisha marabi yaani ile ya Eden au paradisi ya ulimwengu ujao baada ya kifo.

Kumbe, Mungu anataka watoto wake waishi kwa furaha hapa duniani katika mazingira ya sikukuu, ya sherehe za ndoa, mazingira ya furaha na ya upendo. Unapoutazama ulimwengu wa leo, huwezi kuiona picha hii ya paradisi ya Eden ya karamu na ya sherehe, yaani karamu ya mahusiano mapya, ya furaha ya sherehe ambayo yanawakilishwa na karamu ya ekaristi takatifu. Kwa vyovyote hatuwezi kusema kuwa ulimwengu huu ni wa watu wanaosherehekea arusi kama tusikiavyo katika injili ya leo, badala yake tunaona na kusikia juu ya vita kila mahali, tunaona watu waliokata tamaa, wakimbizi, madhulumu, kukandamizana, nk.

Kumbe ukweli wa mambo, ulimwengu huu ni bustani ya paradisi ambayo Mungu ameiandaa, nasi binadamu wote tumealikwa kuingia kuifaidi. Kinyume chake tunawaona waalikwa wachache ndiyo wanaofaidi mnuso, kwa sababu wamejibinafsisha ulimwengu huu, wamewatenga waalikwa wenzao na mbaya zaidi wamemsahau hata mwandaaji wa mnuso huu.

Mtayarishaji wa mnuso wa arusi katika mfano wa leo ni Mungu mwenyewe. Yeye anataka wanawe waishi katika ulimwengu huu kama vile wangekuwa arusini. Yaani kuishi kwa amani na upendo na kuufaidi pamoja ulimwengu huu. Hapa ndipo linapoingia suala la endapo waalikwa wanakubali mwaliko wa kuja kuungana pamoja, kujenga mahusiano ya kisherehe na ya furaha ya pamoja katika karamu hii ya ufalme mpya inayowaunganisha watu wote, yaani kujenga mahusiano kati ya watu katika ulimwengu huu. Kinyume na kuendeleza ulimwengu wa kale wa kuishi kila mmoja kivyake na kibinafsi. Yesu peke yake alitoa wazo hili la ulimwengu mpya wa mnuso wa arusi ulio tofauti na ulimwengu wa kale. Katika ulimwengu huo wa kale waalikwa wengine hawajisikii kwa sababu waalikwa wenzao wamejimilikisha na kuutamalaki ulimwengu wote. Wamemiliki vyakula vyote, mamlaka yote, mali asili yote nk.

Hapa ndipo unapoona sababu ya hali halisi ya kuwepo kwa vita na magomvi katika ulimwengu. Kutokana na vurugu hizo, hali ya hewa ya karamu au sherehe inabadilika. Mnuso unageuka kuwa mnuko. Kumbe karamu iliandaliwa ili kutosha wote endapo kungekuwa na ustaarabu, lakini bila utaratibu chakula hakitatosha kwa wote kwani kimevamiwa na wachache wenye ubinafsi. Vurugu hilo linafanywa na wale wanaochukua chakula bila kufuata utaratibu wa haki na upendo kadiri ya malengo ya mwandaaji yaani Mungu.

Kwa hiyo, mfano huu unahusu mahusiano ya walioalikwa kwenye kutumia mali ya ulimwengu huu kwa haki ili kutosha kwa wote, ili wote wawe na furaha. Masilahi ya ulimwengu huu (sherehe hizi za arusi) ni mengi na yametayarishwa ili kuwatoshea wote. Huu ndiyo ulimwengu mpya wa ufalme mpya wa Mungu nasi sote tumealikwa kuuishi na kuufurahia.

Kuna makundi matatu ya watumwa waliotumwa kutawanya mialiko. Makundi mawili ya mwanzoni yanatumwa kwa awamu. Watumwa hawa ni manabii wa agano la kale. Bwana anasema: “Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. Lakini waalikwa hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mwingine kwenye biashara zake, na wengine waliwakamata watumwa wale wakawatenda jeuri hata kuwaua.”

Watumwa hawa wanadhulumiwa na kuuawa kwa sababu katika ulimwengu wa kale, wale waliokuwa na mashamba makubwa na mapana na shughuli na miradi yao, walikuwa na nguvu, na uwezo na walikuwa matajiri. Hao hawakuwa na haja ya kwenda kwenye minuso, kwani walisharidhika na maisha yao. Hivi hawakutaka hata kuingia katika ulimwengu mpya bali wakaamua kubaki katika ulimwengu wao wa kale, ulimwengu wa binafsi siyo wa kushirikiana mambo.

Kwa hiyo, endapo watumwa waliwakera na kuwabugudhi mno, wakawafukuzilia mbali, na wakati mwingine waliweza hata kuwaua. Hivyo ndivyo walivyofanyiwa manabii wa kale. Watu hao walielewa vizuri sana mwito huo wa kuingia arusini, uliowadai kuachana na ulimwengu wa kale na kuingia katika ulimwengu mpya wa haki na upendo. Yaani ulimwengu wa kusherekea mnuso pamoja.

Kabla ya sehemu ya pili ya mfano, yaani ya kuingia kundi la watumwa kwenda kutawanya kadi za mwaliko kwa awamu ya tatu, kimeingizwa kituko kimoja kinachovuruga mfululizo mzuri wa mfano. Kipengee hicho chasema hivi: “Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha kawaambia watumwa wake, arusi i tayari lakini walioalikwa hawakustahili.” Sehemu hii inasimama peke yake na ina maana ya peke yake. Sehemu hiyo ni somo la kitaalilimungu juu ya kile kilichotokea Yerusalemu. Mji wa Yesusalemu unawakilishaa mapato ya kukataa mapendekezo na mwaliko wa kushiriki mnuso wa ufalme wa Mungu, yaani kushiriki karamu, wa kuacha udhulumu.

Kutokana na kukataa huko hata Yesu akasema halitasalia jiwe juu ya jiwe. Ndipo sehemu hiyo ikaingizwa, kama vile ungekuwa adhabu, au laana kutokana na kumkataa Kristu. Lugha hii kali inaakisi lugha ya Agano la kale, ambako makosa, dhambi inaoneshwa kuwa itakuja kuadhibiwa vikali na Mungu, kumbe ukweli wa mambo Mungu haadhibu, bali hayo ni mapato ya dhambi kwa mtu mwenyewe anayeitenda. Pale tunapomkataa Kristu tunajiadhibu wenyewe. Hayo ndiyo mapato ya dhambi.

Kwa namna hiyo, tunaweza kutafakari ulimwengu wa leo na matukio yake juu ya dhambi. Ujumbe muhimu ni kwamba, yule anayekataa mapendekezo ya Kristu, mapato yake unayaona jinsi limwengu unavyoenda. Madhulumu, vita, maangamizi, uonevu, kutoelewana, magomvi katika famili, mashindano nk.

Baada ya kituko hicho cha mji wa Yerusalemu, sasa tukione kikundi cha tatu ambacho mfalme anakiagiza tena: “Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.” watumwa hawa wa kundi la tatu ndiyo mitume na sisi pia. Hao ni watumishi wapya wa Agano Jipya. Watumishi hawa wanaenda kuwaalika watu wote wema na wabaya, vilema, maskini, na wapita njia, watu wenye shughuli zao, yaani wapagani.

Hapo kunakuwa na timbwili la watu wa kila aina. Tungetegemea sasa lango la jumba la sherehe lingefungwa na sherehe zianze. Ndivyo itakavyokuwa katika ulimwengu ujao ambao walioingia paradisini watakuwa wameshaingia, milango itafungwa na mnuso unachukua kasi yake. Kumbe hii ni sherehe au paradisi ya hapa duniani, milango haifungwi, mapato yake kunatokea kasheshe nyingine mle jengoni.

Hebu fuatilia jinsi ilivyokuwa. Mfalme akaingia na kuwakagua walioalikwa. Kisha akamwona mwalikwa mmoja asiye na vazi la arusi akaanza kumwandama. Akaamrisha wamfunge na kumtupa nje. Kulikoni, kwani yeye alikuwa kati ya waalikwa wa mitaani, na waliokuwa katika misafara yao wasingeweza kujiweka sawa kabla. Halafu mbaya zaidi, humo walialikwa watu wa kila aina na wenye mivao tofauti tofauti lakini sasa anaadhibiwa mtu kutokana na kutokuvaa vazi la arusi tu.

Ndugu zangu sehemu hii imekaa safi tu. Kwanza sehemu hii haina muunganiko na sehemu iliyopita, imekaa peke yake na ni mfano wa peke yake ulioletwa ili kutoa tafsiri hii, kwamba unaweza kuingia kwenye karamu lakini unazo bado fikra za kale, na ya vigezo vya kale, hilo ndilo vazi la kale na siyo sare ya mnuso mpya wa arusi. Yawezekana kuwa wewe ukajisikia uko ndani ya mnuso, ndani ya kanisa, lakini kumbe ukweli unaendelea kufikiri na kuishi kama wale walio nje.

Hivi uwepo wako mle ndani ni wa nje tu. Lugha hii ni kwa ajili ya kumwonya mhaini, iwe wa dini au wa chama au serikali, mtu anayejifanya yuko ndani kumbe fikra zake ziko nje. Ndiyo maana Yesu anahitimisha “Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.” Wote wamealikwa, tena wako wengi wanaoingia katika chumba cha arusi, lakini ni nani hasa ameitwa au ameelewa na amepokewa katika mnuso wa arusi mpya aliyoiandaa Mungu kwa ajili ya mwana wake Yesu Kristu na ulimwengu mpya.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.