(Vatican Radio) Baba Mtakatifu Francisko , Jumapili akihutubia mahujaji na wageni
wakati wa sala ya Malaika wa Bwana alisema, "wema wa Mungu," haujui mipaka wala kubagua
dhidi ya mtu yeyote, kila mtu anapewa nafasi ya kuitikia mwaliko wake, wito wake na
kumwamini..
Hotuba ya Papa ililenga katika somo la Injili la Jumapili, kutoka
Injili ya Matayo, ambamo mna mfano wa Mfalme anayetoa mwaliko wa Sikukuu ya harusi,
ambamo waalikwa hawakuhudhuria na hivyo mwaliko unatolewa kwa wote, baadhi wanakubali
na wengine kukataliwa.
Aliendelea kusema kwamba "hakuna hata mmoja kati ya
wale waliochaguliwa kwanza, waliokubali kushiriki katika sikukuu hii. Kila mmoja
alikataa kwa sababu zake, kwamba tayari alikuwa na mpango mwingine, na wengine walionekana
kutojali tu na hata kukerwa na mwaliko waliopewa. Papa aliendelea kueleza, licha ya
mwaliko kukataliwa, Mfalme hakukata tamaa, wala kuifuta sherehe , badala yake alitoa
mwaliko huo kwa watu wote hata nje ya mipaka yake yote , na kuwatuma watumishi wake
waende katika mitaa yote na katika njia panda zote, kuwakusanya wote watakao patikana.
Papa
Francisko kisha alifafanua kwamba huku ni kukataliwa kwa Injili na baadhi ya watu,
na bila kutarajia Injili inahubiriwa kwa watu wote, wote wakipewa mwaliko wa kushiriki
katika Ibada. Hivyo wema wa Mungu, unaonekana kutokuwa na mipaka na wala ubaguzi dhidi
ya mtu yeyote, kila mtu anapewa nafasi ya kuitikia mwaliko huu.
Aliendelea
hii ina maana kwamba, tunahitaji kufungua mioyo yetu kwa wote hata walio pembezoni
mwa jamii, na kutambua kwamba, hata wale waliosahaulika pembezoni, au wale wanao
dharauliwa na kukataliwa na jamii, mbele ya Bwana wote wanathamani kubwa kwa kuwa
Bwana, Mungu wa Upendo na wote wameumbwa kwa ukarimu wa Mungu.
Baba Mtakatifu
Francisko baada ya sala ya Malaika wa Bwana, alielekeza mawazo yake kwa watu waliofikwa
na maafa ya maporomoko ya aridhi huko Genoa, Kaskazini mwa Italia, akionyesha, kiroho,
kuwa pamoja nao, katika mahangaiko na mateso ya wote walio athirika kwa maafa hayo
hasa walio poteza makazi na mali pia.
Katika kujali hali ya watu hawa, siku
ya Jumamosi, Papa Francisko, alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Askofu Mkuu
wa Genoa, Kardinali Angleo Bagnasco, ambaye Ijumaa mara baada ya kupata taarifa za
mafuriko, aliondoka na kuuacha Mkutano wa Sinodi, na kwenda kushirikiana na wenzake
wakati huu wa mateso makubwa ya watu katika mji wa Genoa. Maafa haya yanaweza kuwa
mabaya zaidi kutokana na mvua kubwa kuendelea kunyesha katika eneo hilo la Kaskazini
mwa Italia. Na imesikitisha zaidi kwamba, mafuriko haya yametokea wakati watu wako
katika hatua za kujiinua baada ya kukumbwa na maafa kama haya miaka mitatu iliyopita.
Hivyo juhudi zao zimerudisha nyuma.
Aidha Papa Francisko wakati huo wa Sala
ya Malaika wa Bwana, alilikumbuka tukio la kutangazwa kuwa Mwenyeheri, Mtumishi wa
Mungu Padre Francesco Zirano, aliyeuawa kikatili kwa kukataa kukana imani yake na
badala yake aliongeza uaminifu wake kwa Kristo. Papa amemtaja kuwa ni mfano mzuri
wa kuigwa na wafuasi wote wa Kristo, hasa katika mazingira ya mateso makali yanayotokana
na kuwa Mkristo. Mwenye Heri mpya Padre Francesco Zirano, ametajwa kuwa shujaa
wa Injili.