2014-10-11 08:43:59

TAFAKARI YA NENO LA MUNGU DOMINIKA YA 28 YA MWAKA A, 12OKTOBA


Karibuni tusafiri pamoja katika bahari ya tafakari, chakula cha roho zetu, meza ya neno la Mungu, Dominika ya 28 ya mwaka A wa Kanisa. Tunaalikwa kuwa tayari daima kushiriki karamu ya Bwana iliyo na uzuri wa kila aina. Hata hivyo kushiriki karamu hiyo kwatudai vazi rasmi, kadi ya kiingilio na ndiyo kusema mapendo kwa jirani na kwa Mungu.


Karamu ya Bwana kadiri ya nabii Isaya itafanyika mlimani yaani palipotukuka, palipo na hewa safi, na palipo na usalama kwa hivi kuna amani tele. Nabii anawatayarisha wana wa Israeli watambue kuwa siku moja wataondolewa katika utumwa wa Babeli, watapata furaha na kushangilia wanaporudi nyumbani. Nabii anawafundisha juu ya ujio wa Masiya atakayewaondoa katika makandamizo ya mwovu na hivi itakuwa furaha kuu ambayo nabii Isaya anaiona lazima ifanyike mlimani. Mlima ni ishara ya utukufu wa Mungu, kumbe karamu hii inafanywa na Bwana wa majeshi. Mpendwa msikilizaji habari hii ni ya furaha kwako na kwangu kwa maana ni tangazo la kujaliwa neema iletayo furaha ya moyo, iletayo umoja na ushirika kamili katika familia zetu, ni kuunganika na Kristu katika sakramenti zake na Neno lake lililo la milele.


Baada ya kusikia tangazo la nabii Isaya, iliyo ya furaha, tuone kama kweli habari hii inagusa maisha yetu, tukijiuliza maswali haya: Mbona katika nchi yetu bado kuna shida kama vile mgawo wa umeme ambao ni chukizo kwa maisha ya watu? Mbona kuna machafuko ya hapa na pale katika siasa na maisha kwa ujumla? Je habari hii ya furaha inayonafasi katika mazingira kama haya? Mpendwa msikilizaji, ujumbe huu ni wa maana sana katika nchi yetu. Kwa nini? Ni kwamba habari ya furaha ni ujio wa Masiya ajaye kwa amani na hivi anakutaka wewe unayeshiriki maisha ya jamii kama mwanasiasa, kama kiongozi kama mkristu uanze polepole kuleta mapinduzi ya kiroho na hapa ndipo karamu yenye vitu vinono inaanzia. Kumbukeni kuwa Mungu anataka tushiriki utukufu wake tukiwa huru kabisa na hivi ni kazi yetu kuweka bidii kujenga misingi ya haki na amani. Kazi ya amani na furaha ni tunda la Roho Mtakatifu. Kumbe ujumbe wa Mtume Paulo unatusaidia kuelewa hilo anaposema nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu, ndiyo kusema yafaa kumshirikisha Roho Mtakatifu ili kazi ya kujenga amani iweze kuwa ya mafanikio na hivi furaha ienee ulimwenguni kote.


Mwinjili Mathayo anakazia ujumbe wa nabii Isaya juu ya karamu akisema maisha ya Kikristu ni arusi ambayo watu wote wamealikwa, lengo likiwa ni kushiriki ufalme wa mbinguni. Maisha ya Kikristu ni furaha tele ambayo huja kwa sababu kuna kila aina ya vyakula na mashangilio, ndiyo kusema neema ziletwazo na ushiriki mkamilifu katika hazina za Kristu kwa mastahili ya msalaba. Kumbe anataka watu wote washiriki na kila siku anatuma wajumbe wake kupeleka mwaliko kwa kila mmoja wetu. Mpendwa msikilizaji, pamoja na mwaliko wa Mungu, oneni kiburi cha mwanadamu mbele ya mwaliko huo, mwanadamu anathubutu kusema niko katika biashara zangu, niko shambani mwangu na hata wakati fulani kujibu mwaliko kwa matusi makali! Sijui kama haya yako katika jumuiya zetu, katika nchi yetu na zaidi katika familia yako! Yafaa kuangalia vema.


Mwinjili anaendelea kutufundisha juu ya mwaliko wa Mungu kuwa tunahitaji kuitika kwa upendo na uhuru kamili ili tupate nafasi ya kuangalia mahitaji gani tupaswayo kuwa nayo. Ndiyo kusema mwaliko huanza kuonekana kwa njia ya ubatizo na polepole mambo ambata hufuata ambayo yadai toba na ukaguzi wa amara kwa mara. Katika hili tunagundua kwa nini mmoja aliyeingia katika karamu alitolewa nje na kupewa adhabu kali. Huyu hakujali maisha endelevu, ni kama aliyebatizwa na baadaye hafanyi bidii ya kumjua Bwana, kupokea na kujifunza mausia ya Kanisa na jumuiya anamoishi, na badala yake huona kama kubatizwa kunatosha. Mpendwa msikilizaji, ubatizo ni msingi lakini hautoshelezi wokovu kama mmoja hawajibiki katika mambo yahusuyo mapendo kwa jirani. Kumbe vazi rasmi ni shughuli za upendo zilizo matunda ya uadilifu katika maisha yako ya kila siku. Ndiyo kusema, yafaa sasa kuanza safari ya maandalizi ili kununua vazi la arusi na gharama yake ni kubwa lakini kila mmoja wetu anao uwezo wa kuipata, ndiyo upendo, ndiyo maisha ya jumuiya, ndiyo maisha ya kuvumiliana katika ndoa, kuvumiliana katika maisha ya kichungaji.


Mpendwa mwanatafakari, ninakusindikizeni nikikutakia heri na baraka za Mungu ili ukue katika zawadi ya upendo, upendo usiochakachuliwa bali adilifu uliojaa hekima ya kimungu na hivi utakuwezesha kuingia katika karamu ya ufalme wa mbinguni.
Tumsifu Yesu Kristu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps








All the contents on this site are copyrighted ©.