2014-10-07 15:59:13

Tuzitazame fadhila za hekima na busara katika maisha yetu .


Mpendwa wa kipindi cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Tuhitimishe makala yetu juu ya fadhila za hekima na busara. Lengo letu: tunataka tujiunde hivi ili hekima yetu, ujuzi wetu wa mambo, elimu yetu, idhihirike katika namna yetu ya kuishi. Hekima ni nyenzo ya maisha bora, hekima ni lulu kuu kupita zote.

Ndiyo maana mfalme Sulemani alipoambiwa na Mungu aombe chochote, hakuomba kingine isipokuwa hekima. Hekima kama elimu ya mambo katika uhalisia wake, ndio dira ya kuongoza maisha yetu. Hata kama tungekuwa na utajiri wa mali, tukikosa hekima katika kuitumia, basi mali hiyo inageuka kuwa sumu ya kutuangamiza sisi wenyewe na kuwahatarisha wengine. Ndio maana si mara chache tunaaswa, kwamba urithi mzuri kwa waana ni hekima/elimu.

Na tuzitazame fadhila za hekima na busara katika maisha yetu ya kila siku. Sote katika maisha tunaalikwa kuitafuta hekima. Na hekima hiyo yenye kutupatia sisi uhuru na usalama, si nyingine bali ni hekima ya kimungu. Neno la Mungu linasema “Hekima huwatukuza wanawe na kuwasaidia wale wanaomfuata. Ampendaye hekima anapenda maisha, wamtafutao hekima mapema watajazwa furaha...Bwana awapenda wale wapendao hekima” YbS. 4:11-14.

Hekima hiyo ya kimungu, itusaidie sasa katika maisha yetu. Itusaidie kuishi vema sisi wenyewe na kuishi vema na jumuiya ya watu popote. Neno latuambia “ ifanye jumuiya ya watu ipendezwe nawe” (YbS. 4:7. Ni kwa hekima na busara tu ndiyo twaweza kuwa wapendevu mbele za watu. Hekima inatupatia nini cha kusema. Busara inatuelekeza ni wapi tuseme, lini tuseme na kwa nani tuseme na nama gani tuseme. Tunaambiwa “usiache kusema wakati unaofaa, wala usiifiche hekima yako” YbS 4:23.

Mintarafu mazungumzo, busara ya maisha inatuelekeza hivi, kila mtu anapaswa kusema ukweli, lakini sio kila ukweli unasemwa kwa kila mtu, na tena sio kila ukweli unasemwa kila mahali, na tena, sio kila ukweli unasemwa na kila mtu, na tena sio kila ukweli unaoujua lazima uusema, na zaidi sana sio kila jambo linalokusibu lazima ulitangaze kwa watu. Tunaambiwa “usimfungulie kila mtu yaliyomo moyoni mwako” (YbS 8:19). Jilinde, Yoshua Bin Sira anasema “tunza siri zako na uwe mwangalifu, maana unatembea kwenye hatari” 13:13.

Hapa kinachodaiwa zaidi ni busara katika matumizi ya mdomo wako. Busara hiyo itakulinda. Mintaraufu kusema sema, neno la Mungu linatuasa “usipepete nafaka kwa kila upepo...uwe mwepesi kusikiliza lakini uwe mwangalifu katika kutoa jibu” YbS 5:9-11. Ndipo hapo tunaambiwa, sio kila swali binafsi unaloulizwa lazima ulijibu. Kama wewe sio msemaji mkuu wa jambo unaloulizwa, ni aheri kukaa kimya, sija baadaye ukashindwa kuyawajibikia maneno uliyoyasema.

Hekima inatuambia ni vema kuwa na marafiki. Busara ituelekeze namna gani tuwapate marafiki na namna gani tuishi nao. Tupo ambao tuna uzembe uliopitiliza, kila rafiki ajaye tunamwambia siri zetu zoote. Kesho na kesho kutwa urafiki unapoingia dosari, basi moyo wako wote unaanikwa mtaani. Tunahitaji kuwa na busara kubwa katika mahusiano, tuwe waangalifu sana, hasa kwa hao unaowaita marafiki sako. Neno la Mungu linasema “ukitaka kupata rafiki, mchunguze kwanza, usiharakishe kumwamini” YbS 6:5-17. Sasa tupo wenye bahati mbaya ambao, unamfahamu mtu kwa siku mmoja tu, na siku hiyohiyo anakuwa rafikia yako, na unamweleza siri zako na mipango yote. Kufanya hivyo ni kuiweka heshima yako hatarini.

Hekima inatupatia jambo la kutenda. Busara inatuelekeza, wapi tutende, lini tutende na katika mazingira gani tutende. Uzembe katika matendo daima umewafedhehesha wakuu. Kuna wakati tumejisingizia kuwa sisi ni binadamu na hivyo tuna lazima ya kuwa wawazi. Ikumbukwe kwamba ubinadamu sio tiketi ya uhovyo. Tuwapo katika jamii adilifu ni lazima kabisa kuheshimu matakwa ya aibu. Hatuwezi kujiachia tu katika matendo ya aina zote bila kujali mazingira wala wakati. Kufanya hivyo ni kujiaibisha mwenyewe na kukwaza watu pia.

Nyakati zetu hizi za utandawazi, tunadaiwa kujilinda zaidi. Hekima yetu ituambie wazi kuwa tupo katika nyakati si salama sana kimaadili. Busara ituelekeze namna ya kuenenda ili tusijizolee aibu isiyofutika maishani. Katika ulimwengu wetu huu, kuna vitu vingi vizuri sana, lakini sio kila kitu kizuri kinafaa! Wapo watu wengi wazuri sana, lakini sio kila watu wazuri ni wema mioyoni. Busara ituelekeze namna sahihi ya kutumia vyombo vya mawasiliano kwa kulinda zaidi utu na heshima ya mwanadamu. Kwa sababu ya kukosa hekima ya kimungu na busara stahiki, leo hii vyombo vya mawasiliano, kama vile simu za mkononi, tv hata kamera vimekuwa ni vyombo vya kurarua utu na heshima ya mtu.

Hapa tunasema tena kwamba, kwa busara yako, kamwe usitumie mtandao ili kuuponda utu wa mtu kwa kumuanika katika ufaragha wake. Kila mtu ana haki ya faragha. Ila maadili yatukumbushe kwamba, tunahitaji faragha adilifu. Lakini pia kwa busara, ni wajibu wa kila mmoja kujilinda ili usinaswe na waliofilisika maarifa. Ndipo hapo tunakumbushia wito wa kijiwekea miiko katika maisha. Uwe na mwiko wa mazingira, yaani usipende kuwa kila mahali. Tena, uwe na mwiko wa mahusiano, yaani usipende kuwa rafiki ya kila mtu, usipende kumkaribisha kila mtu katika faragha yako, utaanikwa mtaani na haitafutika. Tena, uwe na mwiko wa vyakula na vinywaji. Kwa busara ukijiwekea makatazo binafsi ya maisha, utajiokoa na majanga mengi sana.


Lakini hilo lawezekana zaidi kwa msaada wa Mungu. Tunaambiwa “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako” (). Na daima tusali na mzaburi tukisema “Ee Bwana, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako, Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu. Zab. 25:4- 5.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.